Nov 02, 2018 07:28 UTC
  • Rais Mnangagwa: Zimbabwe ina hifadhi kubwa ya mafuta na gesi

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe amefichua kuwa, nchi hiyo ina hifadhi kubwa ya mafuta na gesi katika mji wa Muzarabani ulioko kaskazini mwa nchi.

Rais Mnangagwa alibainisha hayo jana Alkhamisi katika kikao na waandishi wa habari jijini Harare na kuongeza kuwa, taifa hilo litafikia hatua ya kuanza kuchimba visima vya bidhaa hizo muhimu kufikia katikati ya mwaka 2020 na kwamba utafiti wa kuvumbua visima zaidi unaendelea.

Kwa mujibu wa rais wa Zimbabwe, uvumbuzi wa bidhaa hizo umefanywa na kampuni ya nishati ya Australia inayofahamika kama Invictus. Invictus katika miezi ya hivi karibuni imekuwa ikiendeleza utafiti wa mwanzo uliofanywa katika miaka ya 90 na kampuni ya Marekani ya ExxonMobil ambayo huko nyuma ilifahamika kama Mobil.

Kampuni hiyo ya Australia ambayo imekubaliana na serikali ya Harare kuhusu namna ya kugawana mapato ya bidhaa hizo inawekeza dola milioni 20 katika uchimbaji wa kisima cha kwanza cha bidhaa hizo.

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe

Rais Mnangagwa anakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kukomesha hali ya kutengwa Zimbabwe kimataifa na kurekebisha uchumi dhaifu wa nchi hiyo unaoyumba kutokana na ukosefu wa ajira na uhaba wa fedha za kigeni.

Zimbabwe inakabiliwa na changamoto hizo za kiuchumi na uchochole licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili, kama vile madini ya dhahabu, almasi, makaa ya mawe, chuma, shaba na platinamu.  

Tags