UN: Sudan inapasa kuwashtaki wahusika wa jinai za Darfur
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49208-un_sudan_inapasa_kuwashtaki_wahusika_wa_jinai_za_darfur
Umoja wa Mataifa umeitaka Sudan kuwafungulia mashtaka askari jeshi waliohusika na mashambulizi jimboni Darfu magharibi mwa nchi hiyo kuanzia mwaka 2014 hadi 2016.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 02, 2018 23:25 UTC
  • UN: Sudan inapasa kuwashtaki wahusika wa jinai za Darfur

Umoja wa Mataifa umeitaka Sudan kuwafungulia mashtaka askari jeshi waliohusika na mashambulizi jimboni Darfu magharibi mwa nchi hiyo kuanzia mwaka 2014 hadi 2016.

Umoja wa Mataifa pia umeitaka Suda ishirikiane na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ambayo ilitoa waranti wa kumtia mbaroni Rais Omar al Bashir wa nchi hiyo kwa tuhuma za kufanya jinai za kivita.

Rais Omar Hassan al Bashir wa Sudan

Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ilipitia upya rekodi ya Sudan na wiki hii ikatoa majumuisho yake. Kamati hiyo imesema kuwa, mauaji ya kusulubu na kuwapiga mawe watu hadi kufa yanapaswa kufutwa katika sheria za nchi hiyo na kwamba maafisa wa serikali ya Sudan wanapasa kuacha kuwafungulia mashtaka na kuwatisha waandishi habari, wakosoaji na wanaharakati.

Maelfu ya watu waliuliwa katika vita vya ndani nchini Sudan vikiwemo vile vilivyojiri katika jimbo la Darfur magharibi mwa nchi hiyo tangu mwaka 2003 ambako waasi walikuwa wakipigana dhidi ya serikali ya Rais al Bashir.

Kamati hiyo ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa inasikitisha kuona kwamba si tu kuwa Sudan imeshindwa kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria wahusika wa jinai zilizotajwa kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo bali Khartoum imekataa pia kushirikiana na mahakama ya ICC ambayo ilitoa waranti wa kutiwa mbaroni raia na maafisa wa nchi hiyo wanaotuhumiwa kufanya mauaji ya kimbari, jinai dhidi ya binadamu na jinai za kivita.