Kiir kuwa mpatanishi baina ya serikali ya Sudan na waasi wa Darfur
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49270-kiir_kuwa_mpatanishi_baina_ya_serikali_ya_sudan_na_waasi_wa_darfur
Serikali ya Sudan imetangaza kuwa, Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini atakuwa mpatanishi katika mazungumzo ya amani baina ya Khartoum na waasi wa eneo la Darfur.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 04, 2018 08:55 UTC
  • Kiir kuwa mpatanishi baina ya serikali ya Sudan na waasi wa Darfur

Serikali ya Sudan imetangaza kuwa, Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini atakuwa mpatanishi katika mazungumzo ya amani baina ya Khartoum na waasi wa eneo la Darfur.

Taarifa iliyotolewa na serikali ya Sudan imesema kuwa, Khartoum imekubali pendekezo la Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini kuwa mpatanishi baina ya Khartoum na waasi wa eneo la Darfur lililoko magharibi mwa nchi hiyo. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, uamuzi huo umechukuliwa kwa shabaha ya kupeleka mbele mwenendo wa amani nchini Sudan.

Uamuzi huo umetangazwa baada ya safari ya Naibu wa Rais wa Sudan, Faisal Hassan Ibrahim huko Sudan Kusini. Katika safari hiyo pande mbili ziliafikiana juu ya suala la Kiir kuwa mpatanishi kati ya serikali ya Khartoum na waasi wa Darfur. 

Vita na machafuko ya eneo la Darfur yalianza mwaka 2003 baada ya wakazi wa eneo hilo kuanzisha malalamiko ya kupinga ubaguzi unaofanywa na serikali kuu ya Sudan kwa maslahi ya raia wenye asili ya Kiarabu. 

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, zaidi ya watu laki tatu wameuawa na wengine milioni mbili na nusu wamelazimika kuwa wakimbizi katika eneo la Darfur kutokana na mapigano baina ya waasi na jeshi la serikali ya Sudan.