Wafanya magendo ya binadamu wawaachia huru mateka 84 mashariki mwa Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49612-wafanya_magendo_ya_binadamu_wawaachia_huru_mateka_84_mashariki_mwa_sudan
Maafisa husika wa Sudan wameripoti kuwa mateka 84 raia wa kigeni wakiwemo wanawake 51 wameachiwa huru na kundi moja la magendo ya binadamu katika mkoa wa Kassala mashariki mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 19, 2018 04:29 UTC
  • Wafanya magendo ya binadamu wawaachia huru mateka 84 mashariki mwa Sudan

Maafisa husika wa Sudan wameripoti kuwa mateka 84 raia wa kigeni wakiwemo wanawake 51 wameachiwa huru na kundi moja la magendo ya binadamu katika mkoa wa Kassala mashariki mwa nchi hiyo.

Ilmuddin Messi Mkurugenzi wa Masuala ya Usalama wa Mkoa wa Kassala ameeleza kuwa mateka hao wana umri wa karibu miaka 30 na kwamba 51 kati yao ni wanawake ambao waliingia Sudan wakitokea nchini Eritrea. Ameongeza kuwa watu hao waliokuwa wametekwa nyara wana hali mbaya sana huku wengi wao wakiwa wameteswa na kubakwa. 

Baadhi ya mateka wa Kieritrea walionusurika katika genge la magendo ya binadamu

Messi amebainisha kuwa mateka hao kutokea Eritrea walikuwa wanashikiliwa na kundi hilo la magendo ya binadamu kwa muda wa kuanzia siku kumi hadi miezi miwili huku kundi hilo likitaka kulipwa fedha na familia za wahanga ili kuwaachia huru mateka hao. Wafanya magendo ya binadamu mara kwa mara huwakamata mateka baadhi ya wahajiri haramu huko Sudan na kisha kutaka kulipwa kiasi kikubwa cha fedha kutoka familia zao. Sudan ni moja ya nchi zinazotumika kama kivuko cha wahajiri wa Kiafrika kuelekea Ulaya. Mwaka 2014 bunge la Sudan lilipasisha sheria za kupambana na magendo ya binadamu; sheria ambayo iwapo mtu atapatikana na hatia atahukumiwa kufungwa jela kati ya miaka mitano hadi kumi. Siasa za uingiliaji khususan katika nchi za eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika zimesababisha mgogoro mkubwa wa wahajiri kuwahi kushuhudiwa katika maeneo hayo na kuzipelekea nchi za Ulaya kukabiliwa na wimbi kubwa la wahajiri.