Amnesty yaitaka ICC ifanye uchunguzi kuhusu mateso yanayofanywa na Boko Haram
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50083-amnesty_yaitaka_icc_ifanye_uchunguzi_kuhusu_mateso_yanayofanywa_na_boko_haram
Shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International limeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kufanya uchunguzi wa kina kuhusu ukandamizaji na mateso dhidi ya binadamu yanayofanywa na magaidi wa Boko Haram pamoja na jeshi la Nigeria kwenye operesheni za pande hizo mbili na kuilaumu Abuja kwa kutotekeleza ipasavyo majukumu yake katika kulinda haki za binadamu.
(last modified 2026-01-14T11:42:18+00:00 )
Dec 10, 2018 16:10 UTC
  • Amnesty yaitaka ICC ifanye uchunguzi kuhusu mateso yanayofanywa na Boko Haram

Shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International limeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kufanya uchunguzi wa kina kuhusu ukandamizaji na mateso dhidi ya binadamu yanayofanywa na magaidi wa Boko Haram pamoja na jeshi la Nigeria kwenye operesheni za pande hizo mbili na kuilaumu Abuja kwa kutotekeleza ipasavyo majukumu yake katika kulinda haki za binadamu.

Amnesty International yenye makao yake nchini Uingereza imesema kuwa, serikali ya Abuja imemuweka kwenye wakati mgumu mwendesha mashtaka mkuu wa ICC, Fatou Bensouda kwa kuonesha kuwa iko tayari kuchukua hatua dhidi ya uhalifu unaofanywa na pande zote mbili za magaidi wa Boko Haram na wanajeshi wa Nigeria lakini ukweli ni kuwa serikali ya Rais Muhammad Buhari haichukui hatua zozote za maana.

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, Bi Fatou Bensouda

Mwaka 2010, Bensouda alifungua faili la kesi za jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu, mwaka mmoja baada ya magaidi wa Boko Haram kuanzisha mashambulizi nchini Nigeria mwaka 2009.

Kesi zilizofunguliwa wakati huo ni sita na zilijumuisha mauaji ya raia, kutekwa nyara watu kwa umati, kuvamia shule na maeneo ya ibada, uhalifu wa kijinsia pamoja na kutumia vibaya watoto wadogo. Jeshi la Nigeria linakabiliwa na kesi mbili ambazo ndani yake kuna madai kama ya kushambulia raia, kuwatia mbaroni kwa umati watu wa kawaida na kuwashikilia watuhumiwa, kuwatesa na kuwadhalilisha.

Taarifa ya Amnesty International imekuja siku chache baada ya Fatou Bensouda kusema katika ripoti yake ya kila mwaka ya Disemba tano 2018 kwamba inavyoonekana ni rahisi kufuatilia mashtaka dhidi ya Boko Haram lakini si jambo jepesi kuwafuatilia wanajeshi wa Nigeria wanaohusika katika uhalifu.