Dec 29, 2018 08:02 UTC
  • Watu kadhaa wakiwemo watalii wauawa katika mripuko wa bomu Misri

Watalii watatu wa Vietnam na raia mmoja wa Misri wameuawa baada ya bomu lililotegwa kando ya barabara kuripukia basi lililokuwa likifanya safari ya kitalii karibu na Mapiramidi ya Giza nje kidogo ya mji mkuu wa Misri, Cairo.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri imesema watalii 11 raia wa Vietnam na dereva wa basi raia wa Misri, walijeruhiwa wakati bomu hilo la kujitengenezea liliporipuka jana ya jioni mwendo wa saa 12 na robo kwa saa za nchi hiyo.

Basi hilo lilikuwa limebeba jumla ya watu 16 wakiwemo watalii 14, dereva na mwongozaji wa utalii raia wa Misri.

Hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na hujuma hiyo, ingawaje magenge yenye mfugamano na kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) yamekuwa yakifanya mashambulizi ya aina hii.

Hujuma hiyo inaonekana kuwa ya ulipizaji kisasi, ikizingatiwa kuwa mapema wiki hii magaidi 14 waliuawa na maafisa usalama wa Misri katika mkoa wa Sinai Kaskazini, ulioko kaskazini mwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Basi la watalii liliporipuliwa

Eneo la Sinai huko kaskazini mwa Misri limekuwa likishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara ya makundi yenye silaha dhidi ya wanajeshi na maafisa usalama wa serikali.

Mashambulio hayo yameongezeka baada ya rais wa hivi sasa Abdel Fattah el Sisi kushika hatamu za uongozi mwaka 2014 baada ya kuongoza mapinduzi ya kijeshi yaliyompindua Mohammad Morsi, rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Misri.

Tags