Jan 08, 2019 07:24 UTC
  • Zaidi ya waandamanaji 800 wakamatwa Sudan

Zaidi ya waandamanaji 816 wamekamatwa kote Sudan katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita baada ya kuanza maandamano dhidi ya utawala wa Omar al-Bashir.

Maafisa wa serikali ya Sudan wanasema watu 19 wameuawa, wakiwemo maafisa wawili wa usalama katika maandamano hayo lakini shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International linasema idadi ya waliouawa ni 37.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Sudan Ahmed Bilal Osman amethibitisha Jumatatu kuwa hadi sasa waandamanaji 816 wametiwa mbaroni. Aidha amesema katika maandamano hayo ambayo yalianza Disemba 19, nyumba 118 zimeharibiwa, zikiwemo 18 za Idara ya Polisi huku magari 194 yakiteketezwa kwa moto.

Rais Omar al Bashir wa Sudan

Sudan imekumbwa na maandamano makubwa ya nchi nzima kulalamikia hali mbaya ya kiuchumi na inasemekana kuwa mgogoro kama huo haujawahi kuikumba Sudan katika kipindi cha zaidi ya miaka 30 iliyopita. Raia wa kawaida nao wanaendelea kujitokeza katika barabara za miji mbalimbali ya Sudan na kumtaka Rais al-Bashir aondoke madarakani lakini pia wanalalamikia kupanda kwa bei ya mkate na mafuta.

Rais al-Bashir aliingia madarakani mwaka 1993 na kisheria anatakiwa kuondoka madarakani mwaka 2020 lakini kulikuwa na tetesi kuwa anataka kujiongezea mihula zaidi jambo ambalo limewakasirisha wananchi.

Tags