13 Wauawa katika mapigano mapya nchini Libya
Wizara ya Afya ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya imetangaza habari ya kuuawa watu 13 wengine katika mapigano mapya yaliyotokea kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.
Wizara ya Afya ya Libya imesema katika taarifa yake hiyo kwamba idadi ya watu waliouawa katika mapigano ya kusini mwa Tripoli yaliyoanza tangu Jumatano na kuendelea hadi leo hii, imeshafikia watu 13. Waliojeruhiwa hadi hivi sasa ni watu 52 kwa mujibu wa taarifa hiyo.
Taarifa hiyo pia imeyataka makundi yote yanayopigana yaache kuwashambulia madereva wa magari ya wagonjwa wakati wanapotoa huduma kwenye mapigano hayo.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nao umelaani machafuko hayo mapya ya mjini Tripoli na kutoa onyo kali kwa pande hasimu zinazohatarisha usalama wa mji mkuu huo na wa raia na mali zao.
Libya haijawahi kuwa na utulivu na amani ya hata siku moja tangu mwaka 2011 baada ya Marekani kuongoza jeshi la nchi za Magharibi NATO kuivamia kijeshi nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na kusambaratisha miundombinu yake yote pamoja na kuacha silaha zikiwa zimeenea mikononi mwa makundi hasimu ambayo kila moja linapigania kuwa na nafasi kubwa zaidi hivi sasa nchini humo.