Mazungumzo ya kusaka amani CAR kufanyika Khartoum, Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51005-mazungumzo_ya_kusaka_amani_car_kufanyika_khartoum_sudan
Duru mpya ya mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) na makundi 14 ya upinzani imepangwa kufanyika wiki ijayo mjini Khartoum, Sudan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 20, 2019 10:39 UTC
  • Mazungumzo ya kusaka amani CAR kufanyika Khartoum, Sudan

Duru mpya ya mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) na makundi 14 ya upinzani imepangwa kufanyika wiki ijayo mjini Khartoum, Sudan.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Bw. Al-Dirdiri Mohamed Ahmed amesema, serikali ya CAR na makundi ya upinzani yatashiriki kwenye mazungumzo hayo yatakayofanyika wiki ijayo tarehe 24 Januari.

Mazungumzo hayo, yanayosimamiwa na Umoja wa Afrika, yanalenga kushughulikia masuala ya utawala wa serikali, msamaha, wapiganaji kurudi katika jamii na ushiriki wa vyama vya siasa kwenye utawala.

Agosti mwaka 2018, Sudan ilikuwa mwenyeji wa mazungumzo kati ya waasi wa Anti-Balaka na kundi la upinzani lenye silala la Seleka la Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo ni miongoni mwa nchi masikini zaidi duniani, ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa mwaka 2013 baada ya kuondolewa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo François Bozizé kufuatia hujuma ya waasi wa Seleka. Tangu wakati huo hadi sasa nchi hiyo imekuwa uwanja wa mapigano ya kila uchao kati ya makundi hasimu, hususan lile la Kikristo la Anti-Balaka na kundi la Seleka. Idadi kubwa ya Waislamu wameuawa kwa umati na wengi kulazimika kuwa wakimbizi kufuatia hujuma za genge hilo la Anti-Balaka.