Boko Haram: Tumeua askari 30 kaskazini mashariki mwa Nigeria
Kundi la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram limedai kuwa wanachama wake wametekeleza shambulizi katika eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuua askari 30 wa nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na kundi hilo imesema kwamba, katika shambulizi hilo lililotokea siku ya Jumamosi katika kijiji cha Lumani ndani ya jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, jumla ya askari 30 wa serikali waliuawa. Hii ni katika hali ambayo jeshi la nchi hiyo limetangaza kwamba askari wake walifanikiwa kuzuia shambulizi la wanachama wa genge hilo katika kijiji hicho cha Lumani. Katika taarifa hiyo, jeshi la Nigeria limeongeza kwamba, kwenye shambulizi hilo askari wanane pekee ndio waliojeruhiwa.
Mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka jana, kundi la Bokko Haram lilidhibiti kambi mbili za jeshi la serikali huko kaskazini mashariki mwa Nigeria. Mapigano ya miaka tisa kati ya kundi hilo na jeshi la serikali, yamepelekea zaidi ya watu elfu 27 kuuawa, milioni na laki nane kuwa wakimbizi sambamba na kuibuka mgogogro wa kibinaadamu katikka eneo. Kabla ya hapo, Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria alitangaza kwamba hivi sasa kundi hilo limedhoofika na kushindwa katika uwanja wa kiutaalamu, ingawa Jumatano iliyopita alikiri kwamba mashambulizi ya jeshi la serikali yamefeli mbele ya kundi hilo.