Sherehe za kutiwa saini makubaliano ya Amani CAR sasa kufanyika Jumanne
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51325-sherehe_za_kutiwa_saini_makubaliano_ya_amani_car_sasa_kufanyika_jumanne
Sherehe za kuanza utekelezaji wa makubaliano ya amani baina ya serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na makundi 14 yenye silaha zilizopangwa kufanyika jana Jumapili, zimeakhirishwa na sasa zitafanyika kesho Jumanne mjini Khartoum, Sudan. Mwenyeji wa makubaliano hayo yaani serikali ya Sudan imesema kuwa, saini ya mwisho ya makubaliano hayo itatiwa baadaye, ingawa haikusema ni lini hasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 04, 2019 04:25 UTC
  • Sherehe za kutiwa saini makubaliano ya Amani CAR sasa kufanyika Jumanne

Sherehe za kuanza utekelezaji wa makubaliano ya amani baina ya serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na makundi 14 yenye silaha zilizopangwa kufanyika jana Jumapili, zimeakhirishwa na sasa zitafanyika kesho Jumanne mjini Khartoum, Sudan. Mwenyeji wa makubaliano hayo yaani serikali ya Sudan imesema kuwa, saini ya mwisho ya makubaliano hayo itatiwa baadaye, ingawa haikusema ni lini hasa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan, Babikir al Siddiq amesema hayo katika taarifa yake na kuongeza kuwa, Rais Faustin Archange Touadera wa Jamhuri ya Afrika ya Kati atahudhuria sherehe hizo.

Makundi 14 ya waasi yaliyowakilishwa katika mazungumzo na serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati jana yalitarajiwa kutia saini makubaliano hayo yaliyofikiwa juzi Jumamosi, huku taasisi mbalimbali za ndani na nje zikihimiza kuheshimiwa makubaliano hayo.

Rais Faustin Archange Touadera wa Jamhuri ya Afrika ya Kati

Makundi yote yameelezea furaha yao baada ya kukamilika mazungumzo hayo mjini Khartoum. Baada ya siku kumi za mazungumzo, juzi Jumamosi, Umoja wa Afrika ulitangaza kwamba makundi ya waasi na serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati wamefikia makubaliano. Kila upande umeridhia, lakini haukutoa maelezo zaidi.

Makundi ya watu wenye silaha yanadhibiti karibuni asilimia 80 ya nchi hiyo. Hayo ni makubaliano ya nane ya amani kati ya serikali na waasi huko Jamhuri ya Afrika ya Kati katika kipindi cha miaka saba iliyopita.

Kwa upande wake, afisa wa Umoja wa Afrika AU, balozi Smail Chergui ambaye pia ni kamishina wa tume ya AU ya amani na usalama amesema kuwa, hiyo ni siku na hatua nzuri sana na muhimu kwa Jamhuri ya Afrika ya Kati na watu wake wote na amezitaka pande zote za nchi hiyo kuunga mkono makubaliano hayo.

Amesema, ana matumaini makubaliano hayo ya amani yatawezesha watu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kufuata njia ya maridhiano, umoja na maendeleo.