Viongozi wa Kiislamu nchini Mali wamtaka Waziri Mkuu ajiuzulu
(last modified Mon, 11 Feb 2019 08:00:02 GMT )
Feb 11, 2019 08:00 UTC
  • Viongozi wa Kiislamu nchini Mali wamtaka Waziri Mkuu ajiuzulu

Viongozi na shakhsia wa Kiislamu nchini Mali wamemtaka Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Soumeylou Boubeye Maiga ajiuzulu wadhifa wake, wakisisitiza kuwa serikali yake imeshindwa kukabiliana na jinamizi la ugaidi, Uwahhabi na misimamo ya kufurutu ada.

Viongozi hao walitoa mwito huo jana Jumapili katika Uwanja wa Taifa wa Bamako, wenye uwezo wa kuchukua watu zaidi ya 60,000 kwa wakati mmoja. Makumi ya maelfu ya Waislamu walifurika hadi pomoni kwenye uwanja huo ulioko katika mji mkuu wa nchi hiyo, ambapo wameunga mkono mwito wa viongozi wao wa kidini.

Mahmoud Dicko, Rais wa Baraza la Kuu la Waislamu nchini humo (IHC) aliuambia umati huo kuwa, "Waislamu hawapaswi kuruhusu mambo yaende mrama namna hii, wanatakiwa kuwa macho na kujitolea kwa ajili ya nchi, dini na heshima yao."

Bouye Haidara, shakhsia mwingine wa Kiislamu aliyehutubia hadhira katika mkutano huo wa jana mjini Bamako alisisitiza kuwa, Mali inakabiliwa na tatizo la uongozi, na inahitaji mabadiliko. Amesema lazima wananchi waungane katika vita dhidi ya ufisadi na mmomonyoko wa maadili. 

Magaidi wakufurishaji nchini Mali

Nchi ya Mali ilikumbwa na ghasia na ukosefu wa amani baada ya mapinduzi yaliyotokea nchini humo mwaka 2012. 

Mwaka mmoja baadaye, Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa (MINUSMA) na wanajeshi wa Ufaransa walitumwa nchini humo kwa ajili ya kuwadhaminia usalama raia, lakini vikosi hivyo havijakuwa na utendaji wa kuridhisha katika kurejesha utulivu nchini humo huku vitisho vya ugaidi vikiendelea kuitatiza nchi hiyo.