Middle East Eye: Salah Gosh amefanya mazungumzo ya siri na Israel
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51895-middle_east_eye_salah_gosh_amefanya_mazungumzo_ya_siri_na_israel
Idara ya Ujasusi ya Sudan imekanusha habari iliyotangazwa na Middle East Eye kwamba mkuu wa idara hiyo, Salah Abdallah Gosh amekutana kwa siri na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa shirika la ujasusi la Israel MOSSAD, Yossi Cohen.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Mar 02, 2019 04:36 UTC
  • Salah Abdallah Gosh
    Salah Abdallah Gosh

Idara ya Ujasusi ya Sudan imekanusha habari iliyotangazwa na Middle East Eye kwamba mkuu wa idara hiyo, Salah Abdallah Gosh amekutana kwa siri na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa shirika la ujasusi la Israel MOSSAD, Yossi Cohen.

Awali kituo hicho cha habari cha Middle East Eye cha nchini Uingereza kilifichua kuwa, Salah Abdallah Gosh alikutana kwa siri na Mkurugenzi wa shirika la ujasusi la Israel MOSSAD kandokando ya mkutano wa Usalama wa Munich nchini Ujerumani mwezi uliopita. Kituo hicho kilinukuu duru za ndani ya jeshi la Sudan kwamba, Salah Abdallah Gosh alifanya mazungumzo ya siri na Yossi Cohen katika njama iliyopangwa na nchi za Kiarabu waitifaki wa Israel kwa ajili ya kumuwezesha kushika madaraka ya Sudan baada ya kuondolewa madarakani Rais Omar Hassan al Bashir anayezongwa na matatizo makubwa ya kisiasa na kiuchumi.

Mkutano huo ulitayarishwa kwa siri na Misri, Imarati na Saudi Arabia bila ya Rais al Bashir kujua.

kituo hicho cha habari cha Middle East Eye kinasema, inaonekana kwamba kuna mwafaka jumla baina ya nchi za Kiarabu kwamba Omar al Bashiri ataondolewa madarakani lakini tofauti iliyopo ni juu ya nani atashika madaraka ya Sudan baada yake.

Image Caption

Duru za kipelelezi zinasisitiza kuwa Mkuu wa Idara ya Ujasusi ya Sudan, Salah Abdallah Gosh ana uhusiano mkubwa la Saudi Arabia, Imarati na Misri, witifaki wakubwa wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel. Nchi hizo zinataka Gosh achukue madaraka ya Sudan baada ya al Bashir. Sudan inapitia kipindi kigumu cha ghasia za kisiasa na maandamano ya karibu kila siku yanayomtaka Omar al Bashir ang'atuke madarakani.