Kushadidi mgogoro wa Sudan
Mgogoro wa kisiasa nchini Sudan umeendelea kuchukua wigo mpana kufuatia kuendelea maandamano ya wananchi wa nchi hiyo.
Waandamanaji nchini Sudan wanataka Rais Omar Hassan al-Bashir wa nchi hiyo ajiuzulu na kuachia madaraka na kisha kuundwe serikali ya mpito. Hii ni katika hali ambayo, mapigano mapya katika nchi hiyo yamepelekea zaidi ya watu 50 kuuawa. Katika hali ambayo, Jenerali Kamal Abdul-Maarouf Mkuu wa Majeshi ya Sudan sambamba na kusisitiza juu ya kuweko umoja na mshikamano wa vikosi vyote vya usalama katika kulinda utulivu na uthabiti wa nchi hiyo, amesema kuwa, jeshi halitaruhusu nchi hiyo ikumbwe na mustakabali usioeleweka.
Sudan imekumbwa na maandamano ya kulalamikia hali mbaya ya uchumi na kupanda bei ya bidhaa muhimu hasa mkate na mafuta tangu Disemba mwaka jana. Hata hivyo maandamano hayo baadaye yalichukua mkondo wa kisiasa ambapo sasa waandamanaji wanataka Rais Omar Hassan al-Bashir wa nchi hiyo ajiuzulu na kuachia madaraka. Licha ya vikosi vya usalama kuingilia kati na kuwakandamizaji waandamanaji, lakini maandamano hayo yameendelea kushuhudiwa katika miji mbalimbali ya nchi hiyo hususan mji mkuu Khartoum.
Maandamanao hayo yamechukua mkondo na wigo mpana sasa baada ya vyama vya siasa kujiunga nayo na kutangaza matakwa yao kama kuongezwa uhuru wa kisiasa. Maandamano ya wananchi wa Sudan ni makubwa kiasi kwamba hayajawahi kushuhudiwa mfano wake katika kipindi cha miaka 30 iliyopita. Waandamanaji wanamtuhumu Rais Omar al Bashir na serikali yake kuwa wamevuruga uchumi wa nchi hiyo na wanamtaka yeye na taasisi zote za serikali zing'oke madarakani.
Maandamano hayo yalimfanya Rais al-Bashir avunje baraza la mawaziri tarehe 22 Februari mwaka huu sambamba na kutangaza hali ya hatari kwa muda wa mwaka mmoja, jambo ambalo lilishadidisha ghadhabu za waandamanaji. Sadiq al-Mahdi, kiongozi wa chama cha upinzani cha Umma cha Sudan na kiongozi wa upinzani mtajika nchini humo ametahadharisha juu ya kuendelea mwenendo wa ukandamizaji waandamanaji nchini humo na kusisitiza kuwa, muda mwafaka wa mageuzi umewadia, kwani maandamano haya ya wananchi ni matokeo ya mrundikano wa matatizo ya nchi hiyo.
Hivi karibuni maelfu ya waandamanaji wamekuwa wakijitokeza katika barabara za mji mkuu wa Sudan Khartoum ambapo kwa mara ya kwanza wameandamana na kufanikiwa kufika mbele ya jengo la wizara ya ulinzi ya nchi hiyo ambapo jeshi la nchi hiyo liliwahami waandamanaji hao mbele ya polisi na vikosi vya usalama vya serikali ya Rais al Bashir.
Jenerali Kamal Abdul-Maarouf Mkuu wa majeshi ya Sudan amesema kuhusiana na jambo hilo kwamba, katika hatua ya sasa Sudan inahitajia kuwa macho na kuzingatia kwa pamoja suala la kulinda, utulivu, amani na uthabiti wa nchi na kuzuia kutokea machafuko.
Hivi sasa inaonekana hali ya kisiasa nchini Sudan imekuwa tata zaidi kiasi kwamba, baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti habari ya kuondoka nchini humo Rais Omar Hassan al-Bashir na kukabidhi uongozi kwa jeshi. Hata hivyo baadhi ya viongozi wa Khartoum wamekanusha vikali madai hayo.
Hata kama baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, hali ya sasa ya Sudan ni matokeo ya uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo, lakini inaonekana kuwa, matatizo ya ndani na sera zisizofaa za Rais Omar Hassan al-Bashir ndio chimbuko kuu la malalamiko ya kisiasa na kijamii nchini humo.
Licha ya mabadiko ya hapa na pale yaliyofanywa na serikali, lakini wananchi wa Sudan wanaonekana bado hawajaridhika na wanachotaka wao ni kuondoka madarakani Rais al-Bashir na kuundwa serikali ya mpito kwa shabaha ya kuboresha mazingira ya kisiasa na kiuchumi ya nchi hiyo.
Kushadidi malalamiko nchini Sudan kumeongeza uwezekano wa kuchukua wigo mpana zaidi mapigano ya wananchi na vikosi vya usalama, sambamba na kushadidi ukandamizaji na utumiaji mabavu wa vikosi vya usalama dhidi ya waandamanaji. Inaonekana kuwa, kuendelea kushuhudiwa hali ya sasa, kunazidi kudhoofisha siku baada ya siku uwezekano wa kuendelea kubakia madarakani Rais Omar Hassan al-Bashir ambaye ameiongoza Sudan kwa miongo mitatu.