Rais wa zamani wa Sudan Omar al Bashir apelekwa gerezani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52908-rais_wa_zamani_wa_sudan_omar_al_bashir_apelekwa_gerezani
Rais wa zamani wa Sudan Omar al Bashir anashikiliwa katika gereza ya Kober katika mji mkuu Khartoum lakini bado hakuna taarifa rasmi iliyotolewa kuhusu hatua hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 17, 2019 09:47 UTC
  • Rais wa zamani wa Sudan Omar al Bashir apelekwa gerezani

Rais wa zamani wa Sudan Omar al Bashir anashikiliwa katika gereza ya Kober katika mji mkuu Khartoum lakini bado hakuna taarifa rasmi iliyotolewa kuhusu hatua hiyo.

Duru za familia ya al Bashir zimedokeza kuwa al-Bashir alipelekwa katika gereza hiyo Jumanne na  kwamba amefungwa kifungo cha upweke chini ya ulinzi mkali.

Hata hivyo Baraza la Kijeshi la Mpito ambalo linashikilia madaraka Sudan baada ya al-Bashir kupinduliwa Alhamisi iliyopita bado halijatoa taarifa yoyote ya kuthibtisha au kukanusha kushikiliwa mtawala huyo wa zamani wa nchi hiyo.  Baadhi ya duru mjini Khartoum zinasema Bashir hajapelekwa gerezani na kwamba yuko katika kifungo cha nyumbani chini ya ulinzi mkali akisuburi kupelekwa mahakamani.

Waandamanaji bado wamekusanyika nje ya wizara ya ulinzi mjini Khartoum wakisisitiza kuwa hawataondoka hapo hadi pale watakapomuona al Bashir akiwa amefikishwa kizimbani kujibu mashtaka ya jinai alizotenda katika kipindi cha miaka 30 ya utawala wake.

Maandamano Sudan

Mashuhuda wanasema kuna idadi kubwa ya wanajeshi na askari wa kikosi maalumu nje ya gereza ya Kober kaskazini mwa Khartoum,  jambo ambalo linaloashiria kuwa yamkini al Bashir anashikiliwa hapo.

Hayo yanajiri wakati ambao Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika limeonya kuwa, iwapo Baraza la Kijeshi la Utawala wa Mpito nchini Sudan litashindwa kuwakabidhi raia uongozi katika kipindi cha siku 15 zijazo, Umoja wa Afrika utasitisha uwakilishi wa Sudan katika masuala yote ya umoja huo hadi pale katiba itakapofuatwa.