Wasudan waandamana wakitaka utawala wa kiraia, Saudia, UAE zaunga mkono jeshi
Wiki moja baada ya kupinduliwa rais wa muda mrefu wa Sudan Omar al Bashir, idadi kubwa ya waandamanaji wamekusanyika katika mji mkuu Khartoum wakitaka baraza la mpito la kijeshi likabidhi madaraka kwa raia.
Maelfu ya watu waliandamana mjini Khartoum Alhamisi nje ya wizara ya ulinzi wakipiga nara za 'utawala wa raia." Waandamanaji walionekana wakiwa wamebeba bendera huku wakisisitiza kuwa uhuru na mapinduzi ni chaguo la wananchi. Waandamanaji wanasema wataendelea kubakia barabarani hadi pale raia watakapokabidhiwa mamlaka nchini humo.
Huku wananchi wa Sudan wakiandamana kutaka serikali ya kiraia, tawala za Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zimetangaza kuunga mkono Baraza la Kijeshi la Mpito.
Mkuu mpya wa Baraza la Kijeshi la Mpito Luteni Jenerali Abdel Fattah al Burhan Abdelrahman siku ya Jumanne alipongeza uhusiano wa nchi yake pamoja na Saudi Arabia na UAE. Burhan ana uhusiano wa karibu na wakuu wa Saudia na amepokea ujumbe wa uungaji mkono kutoka kwa wakuu wa Riyadh na Abu Dhabi. Hayo yanajiri wakati ambao siku ya Alhamisi Baraza la Kijeshi la Mpito limemfuta kazi naibu katibu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ambaye alikuwa anapanga safari ya ujumbe wa Qatar kutembelea Khartoum. Qatar ni hasimu wa Saudi Arabia na UAE katika sera za eneo.
Al Bashir ambaye alipinduliwa na jeshi kufuatia miezi kadhaa ya maandamano ya wananchi dhidi ya utawala wake wa karibu miaka 30 huko Sudan sasa anashikiliwa huko Kobar.
Watawala wa kijeshi nchini Sudan wamesema kuwa hawatomkabidhi al Bashir kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ambako anakabiliwa na tuhuma za kufanya mauaji ya kimbari katika jimbo la Darfur ingawa hata hivyo wamesema kuwa atapandishwa kizimbani ndani ya Sudan kujibu mashtaka yanayomkabili.