Sudan yaendelea kukumbwa na maandamano ya kushinikiza kuundwa serikali ya kiraia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52969-sudan_yaendelea_kukumbwa_na_maandamano_ya_kushinikiza_kuundwa_serikali_ya_kiraia
Sudan imeendelea kushuhudia maandamano ya wananchi yanayolitaka Baraza la Kijeshi la Mpito la nchi hiyo kukabidhi uongozi wa nchi kwa raia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 20, 2019 03:36 UTC
  • Sudan yaendelea kukumbwa na maandamano ya kushinikiza kuundwa serikali ya kiraia

Sudan imeendelea kushuhudia maandamano ya wananchi yanayolitaka Baraza la Kijeshi la Mpito la nchi hiyo kukabidhi uongozi wa nchi kwa raia.

Waandamanaji hao wanasisitiza kuwa, Baraza la Kijeshi la Utawala wa Mpito la Sudan linapaswa kukabidhi uongozi wa nchi kwa raia.

Miji kadhaa ya Sudan imeendelea kushuhudia maandamano na migomo ambapo takwa lap kuu ni kukabidhiwa madaraka serikali ya kiraia.

Aidha waandamanaji nchini Sudan wanasisitiza kuwa, wanataka Omar al Bashir apandishwe kizimbani kujibu mashtaka ya jinai alizotenda katika kipindi cha miaka 30 ya utawala wake.

Maandamano ya wananchi wa Sudan

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika hivi karibuni lilionya kuwa, iwapo Baraza la Kijeshi la Utawala wa Mpito nchini Sudan litashindwa kuwakabidhi raia uongozi katika kipindi cha siku 15 zijazo, Umoja wa Afrika utasitisha uwakilishi wa Sudan katika masuala yote ya umoja huo hadi pale katiba itakapoheshimiwa na kufuatwa.

Mgogoro wa Sudan ulianza tarehe 19 Disemba mwaka uliopita ambapo wananchi waliingia mitaani na kuanza kufanya maaandamano ya kila siku kulalamikia ughali wa maisha na hali mbaya ya uchumi pamoja na ongezeko kubwa la bei ya bidhaa na hasa mkate na mafuta. Mgogoro huo ulichukua mkondo mpya wa kisiasa, kiuchumi na kiusalama baada ya jeshi kuingilia kati na kuanza kuwakandamiza waandamanaji.