Wasudan wataka balozi wa Saudia atimuliwe nchini mwao
Baada ya balozi wa Saudi Arabia nchini Sudan kutoa maneno ya uchochezi, kundi moja la wananchi wa nchi hiyo wametaka balozi huyo afukuzwe nchini mwao.
Televisheni ya Russia Today imeripoti habari hiyo na kusema kwamba, kundi hilo la wananchi wa Sudan linalojiita "al Bunyan al Marswus" limetoa mkanda wa sauti unaotishia kumuua Ali bin Hasan Jaafar, balozi wa Saudi Arabia kutokana na kueneza fitna.
Kwa mujibu wa ripoti ya televisheni hyo, hivi karibuni balozi huyo wa Saudia mjini Khartoum, Sudan alisema kuwa nchi yake ndiyo iliyoanzisha na kusimamia mabadiliko yanayotokea Sudan hivi sasa.
Kundi hilo la raia wa Sudan limesisitiza kuwa, Saudi Arabia siyo iliyoleta mabadiliko nchini Sudan bali ni wananchi wa taifa kubwa la Sudan ndio walioleta mabadiliko hayo.
Sudan imekumbwa na maandamano ya nchi nzima ya wananchi tangu tarehe 19 Disemba 2018 yaliyopelekea kupinduliwa utawala wa Rais Omar al Bashir.
Hata hivyo tarehe 11 mwezi uliopita wa Aprili, jeshi la Sudan ndilo lililotangaza kumpindua al Bashir baada ya kushadidi maandamano ya wananchi. Wananchi hao wako mitaani hadi leo hii wakilishinikiza jeshi likabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia haraka iwezekanavyo.
Saudi Arabia inafanya njama za kuhakikisha kuwa wanajeshi wanatwaa madaraka nchini Sudan hasa wale wanaounga mkono mauaji ya kikatili wanayofanyiwa wananchi Waislamu wa Yemen.