Magaidi wa Daesh wadai wameua askari 11 kaskazini mwa Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53427-magaidi_wa_daesh_wadai_wameua_askari_11_kaskazini_mwa_nigeria
Wanajeshi 11 wa serikali wameuawa kaskazini mashariki mwa Nigeria kufuatia shambulio la wanamgambo wanaosadikiwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 12, 2019 02:19 UTC
  • Magaidi wa Daesh wadai wameua askari 11 kaskazini mwa Nigeria

Wanajeshi 11 wa serikali wameuawa kaskazini mashariki mwa Nigeria kufuatia shambulio la wanamgambo wanaosadikiwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS).

Shirika la habari za kipropaganda za genge hilo la ukufurishaji la AMAQ jana Jumamosi liliripoti kuwa, wanachama wake walitekeleza shambulizi hilo dhidi ya kambi moja ya jeshi katika mji wa Gajiganna jimboni Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria siku ya Ijumaa.

Kundi hilo limechapisha picha zinazoonesha kambi ya jeshi iliyoteketezwa kwa moto na miili iliyosambaa kambini hapo wanayodai kuwa ni ya wanajeshi waliowaua.

Vyanzo vya habari zikiwemo duru za hospitali katika eneo hilo zimethibitisha kutokea shambulio hilo lililotekelezwa na magaidi waliokuwa juu ya pikipiki.

Disemba mwaka uliopita, raia 10 waliauawa kaskazini mashariki mwa Nigeria katika shambulio jingine la wanamgambo hao wa Daesh. 

Wanajeshi wa Nigeria jimboni Borno

Aidha Novemba mwaka jana, genge hilo la kigaidi lilidai kuua wanajeshi 100 wa Nigeria katika shambulio dhidi ya kambi moja ya kijeshi mjini Metele jimboni Borno, ingawaje Seneti ya Nigeria ilisema kuwa ni askari 44 tu wameuawa katika hujuma hiyo.

Ifahamike kuwa, jimbo la Borno limekuwa likilengwa kwa mashambulio ya mara kwa mara ya wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram.