UN: Idadi ya waliouawa Darfur nchini Sudan ni watu 17
(last modified Fri, 14 Jun 2019 02:28:47 GMT )
Jun 14, 2019 02:28 UTC
  • UN: Idadi ya waliouawa Darfur nchini Sudan ni watu 17

Umoja wa Mataifa umethibitisha kuwa kwa akali watu 17 wameuawa katika kijiji cha Deleij katikati mwa jimbo la Darfur, magharibi mwa Sudan.

Kikosi cha pamoja cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika UNAMID katika jimbo la Darfur kimetangaza kuwa, watu wengine 15 wamejeruhiwa katika makabiliano baina ya wafugaji wa kuhamahama na wenyeji wa kijiji kilichoshambuliwa.

Awali Kamati Kuu ya Madaktari wa Sudan ilitangaza kuwa watu 11 wameuawa na wengine 20 wamejeruhiwa katika shambulizi la wanamgambo wa 'Janjaweed' wenye mfungamano na jeshi la nchi hiyo katika kijiji hicho cha Darfur. 

Kamati hiyo ilisema wanamgambo hao waliwafyatulia raia risasi hai katika soko la Deleij na kwamba walitekeleza shambuliza hilo dhidi ya raia kwa amri ya jeshi la Sudan.

Askari wa AU na UN jimboni Darfur

Janjaweed ni genge la wanamgambo wa Kiarabu linalotuhumiwa kuua zaidi ya watu laki 3 katika vita vya ndani nchini Sudan vikiwemo vile vilivyojiri katika jimbo la Darfur magharibi mwa nchi hiyo tangu mwaka 2003, ambako waasi hao walikuwa wakipigana dhidi ya serikali ya Omar al Bashir.

Mnamo Juni 3 wanajeshi wa Sudan waliwapiga risasi na kuwaua raia zaidi ya100 ambao walikuwa wamekusanyika na kufanya mgomo wa kukaa chini nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum wakitaka baraza la kijeshi linalotawala nchi hivi sasa liondoke madarakani.