Majenerali wa kijeshi Sudan wakataa uchunguzi wa kimataifa
Baraza la Kijeshi la Sudan limepinga kufanyika uchunguzi wa kimataifa kuhusu mauaji ya umati yaliyofanywa dhidi ya raia waliokuwa wanafanya mgomo wa kukaa kitako mbele ya Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo mjini Khartoum.
Gazeti la "al Sudaniyyah" limemnukuu Luteni Jenerali Shamsuddin Kabashi, msemaji wa Baraza la Kijeshi la Sudan akisema kuwa, baraza hilo linapinga kufanyika uchunguzi wowote wa kimataifa kuhusu mauaji ya watu waliokuwa wanafanya mgomo mbele ya Wizara ya Ulinzi ya Sudan mjini Khartoum.
Luteni Jenerali Kabashi amekiri kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwamba raia waliuliwa katika shambulizi hilo na kusema kuwa, Baraza la Kijeshi lilitoa amri ya kukomeshwa mgomo wa Khartoum lakini raia walikataa hivyo lililazimika kuchukua hatua na huenda katika uchukuaji hatua huo kuna makosa yametendeka.
Amezungumzia pia masharti ya wapinzani ya kutaka wanajeshi warejee kwenye kambi zao kabla ya kufanyika mazungumzo na kusema kuwa, kupunguzwa idadi ya wanajeshi mjini Khartoum kunafanyika baada ya kutathminiwa vigezo vya kiusalama hivyo jambo hilo halina uhusiano wowote na mazungumzo baina ya wapinzani na jeshi.
Aidha amesema kuhusu juhudi za Ethiopia za kuzipatanisha pande hasimu huko Sudan kwamba hadi hivi sasa Addis Ababa haijawasilisha mpango wake katika jambo hilo na kwamba Baraza la Kijeshi liko tayari kupokea na kusikiliza maoni na mapendekezo ya pande zote.
Itakumbukwa kuwa tarehe 3 mwezi huu wa Juni, wanajeshi wa Sudan waliwavamia na kuwashambulia wananchi waliokuwa wamekusanyika mbele ya Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo mjini Khartoum na kuua kwa umati zaidi ya watu 118 na kujeruhi wengine 500. Saudi Arabia, Imarati na Misri ni miongoni mwa nchi zilizotangaza wazi kuliunga mkono Baraza la Kijeshi la Sudan.