Magaidi 42 wa Daesh wauawa katika eneo la Ziwa Chad
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54304-magaidi_42_wa_daesh_wauawa_katika_eneo_la_ziwa_chad
Kikosi cha Pamoja cha Nchi Zinazopakana na Ziwa Chad (MNJTF) kimefanikiwa kuangamiza makumi ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) katika kisiwa cha Doron Naira kwenye ziwa hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 23, 2019 09:19 UTC
  • Magaidi 42 wa Daesh wauawa katika eneo la Ziwa Chad

Kikosi cha Pamoja cha Nchi Zinazopakana na Ziwa Chad (MNJTF) kimefanikiwa kuangamiza makumi ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) katika kisiwa cha Doron Naira kwenye ziwa hilo.

Taarifa iliyotolewa na kikosi hicho imesema kuwa, magaidi 42 waliuawa katika operesheni ya Ijumaa, na kwamba kikosi hicho kimepoteza askari mmoja tu katika makabiliano hayo na magaidi wa Daesh, huku wanajeshi wengine 10 wakijeruhiwa.

Hata hivyo Kundi la Kigaidi la Daesh Magharibi mwa Afrika (ISWAP) ambalo lilijiondoa kwenye genge la Boko Haram na kutangaza utiifu wake kwa ISIS mwaka 2016 limetangaza kuwa limeua wanajeshi 15 wa Kikosi cha Pamoja cha Nchi Zinazopakana na Ziwa Chad katika mapigano hayo ya Juni 21, katika mji wa Garno, jimboni Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria, mpakani na Ziwa Chad.

Magaidi hao hata hivyo hawajaashiria habari ya kuuawa au kujeruhiwa wanachama wake katika shambulizi hilo.

Ramani ya nchi za eneo la Ziwa Chad

Kikosi hicho cha pamoja kimesema mauaji hayo ya wanachama 42 wa Daesh ndilo pigo kubwa zaidi dhidi ya genge hilo la ukufurishaji katika kipindi cha miezi sita iliyopita.

Nchi zinazopakana na Ziwa Chad ambazo ni Nigeria, Chad, Niger, Cameroon na Benin ziliunda kikosi cha pamoja cha kukabiliana na wanamgambo wa Boko Haram na Daesh ambao hadi sasa wameshasababisha maafa makubwa ya roho za watu, mali za umma na kukwamisha maendeleo ya nchi za eneo hilo.