Jeshi la Sudan Kusini lakanusha madai ya UN kuwa limeua raia
Jeshi la Sudan Kusini limekanusha vikali madai ya Umoja wa Mataifa kwamba limeua makumi ya raia wa nchi hiyo katika eneo la Central Equatoria.
Lul Ruai Koang, msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Sudan Kusini (SSPDF) alisema jana Alkhamisi kuwa, jeshi hilo linaheshimu vipengee voyote vya makubaliano ya amani ya Septemba mwaka jana, na kwamba halijaua raia hata mmoja.
Umoja wa Mataifa juzi Jumatano ulitangaza kuwa, zaidi ya watu 100 wameuawa katika mapigano ya hivi karibuni katika nchi ya Sudan Kusini
Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) imetangaza kupitia ripoti yake hiyo kwamba, zaidi ya watu 100 wa pande mbili hasimu wameuawa kufuatia kushadidi machafuko nchini Sudan Kusini tangu kutiwa saini makubaliano ya amani baina ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo na kiongozi wa upinzani Riek Machar.
Aidha ripoti hiyo inaeleza kwamba, raia wa Sudan Kusini wamekuwa wakikabiliwa kwa makusudi na vitendo vya utumiaji mabavu ukiwemo ubakaji kati ya Septemba mwaka jana na Aprili mwaka huu.
Kushadidi machafuko na mapigano huko Sudan Kusini kumewafanya zaidi ya raia 56,000 wa nchi hiyo kuyakimbia makazi yao na kuwa wakimbizi ndani ya nchi hiyo katika kipindi hicho.
Mapatano ya amani yalitiwa saini na pande hizo mbili mwezi Septemba mwaka jana mjini Addis Ababa Ethiopia kwa lengo la kumaliza vita vya miaka sita nchini humo.