Serikali ya Tanzania yalaani matukio ya mauaji nchini Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55197-serikali_ya_tanzania_yalaani_matukio_ya_mauaji_nchini_marekani
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imelaani vikali matukio mawili ya ufyatuaji risasi na mauaji yaliyotokea jana kwa nyakati tofauti nchini Marekani na kusababisha makumi ya watu kuuawa na kujeruhiwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 05, 2019 03:51 UTC
  • Serikali ya Tanzania yalaani matukio ya mauaji nchini Marekani

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imelaani vikali matukio mawili ya ufyatuaji risasi na mauaji yaliyotokea jana kwa nyakati tofauti nchini Marekani na kusababisha makumi ya watu kuuawa na kujeruhiwa.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania imeeleza kwamba, serikali ya nchi hiyo inalaani matukio hayo mawili ya mauaji ya kutumia risasi yaliyotokea jana nchini Marekani.

Aidha serikali ya Tanzania imesema kuwa, ina iman vyombo vya ulinzi na usalama vya Marekani vitachukua hatua madhubuti kuzuia matukio kama hayo yasitokee tena.

Shambulio la Texas Marekani

Ikumbukwe kuwa, watu wasiopungua 10 waliua na wengine 24 kujeruhiwa katika shambulio la ufyatuaji risasi lililotokea jana katika mji wa Dayton, jimboni Ohio nchini Marekani.

Mtu mmoja mzungu aliyekuwa amebeba bunduki aina ya AR 15 alifyatua risasi na kuwaua watu wasiopungua 10 katika mtaa wa Oregon ulioko kwenye mji wa Dayton. Aidha watu 20 waliuawa na wengine 26 walijeruhiwa katika tukio jingine la ufyatuaji risasi lililotokea katika eneo la maduka la Walmart, mjini El Paso katika jimbo la Texas.

Maelfu ya raia wa Marekani huuawa kila mwaka katika matukio ya mashambulizi ya silaha za moto katika maeneo tofauti ya nchi hiyo.

Ushawishi wa lobi zenye nguvu za utengenezaji silaha katika serikali na kongresi ya Marekani umevuruga juhudi zote zinazofanywa na makundi ya kutetea haki za binadamu zinazolenga kubuniwa sheria kali za kudhibiti umiliki wa silaha nchini humo.