Wanigeria wenye hasira walipiza kisasi, wapora maduka ya Waafrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55806-wanigeria_wenye_hasira_walipiza_kisasi_wapora_maduka_ya_waafrika_kusini
Mashambulizi dhidi ya raia wa kigeni huko Johannesburg, Afrika Kusini yameibua hasira kote barani Afrika ambapo maduka yanayomilikiwa na mashirika ya Afrika Kusini yameporwa nchini Nigeria.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Sep 05, 2019 00:09 UTC
  • Wanigeria wenye hasira walipiza kisasi, wapora maduka ya Waafrika Kusini

Mashambulizi dhidi ya raia wa kigeni huko Johannesburg, Afrika Kusini yameibua hasira kote barani Afrika ambapo maduka yanayomilikiwa na mashirika ya Afrika Kusini yameporwa nchini Nigeria.

Taarifa zinasema kuwa, siku za Jumanne na Jumatano, katika mji mkuu Abuja na Lagos, waandamanaji waliokuwa na hasira walipora bidhaa katika maduka makubwa ya Shoprite  ambayo yanamilikiwa na shirika la Afrika Kusini. Aidha maduka ya  Shirika la Mawasiliano ya Simu za Mkononi nchini humo MTN  yanaripotiwa kuporwa katika mji wa Ibadan kusini magharibi mwa Nigeria pamoja na kuwa serikali imetoa wito wa kudumishwa amani.

Nchini Zambia pia wananchi waliokuwa na hasira wameandamana nje ya duka la Pick N Pay linalomilikiwa na shirika la Afrika Kusini. Siku ya Jumapili wimbi jipya la hujuma dhidi ya raia wa kigeni kutoka nchi za Kiafrika lilishuhudiwa tena Afrika Kusini katika miji ya Johannesburg na Pretoria ambapo maduka yanayomilikiwa na wageni hao yameporwa. Polisi Afrika Kusini imetangaza kuwa watu watano wameuawa na kwamba waliohusika na uhalifu huo wamekamatwa.

Raia wa Afrika Kusini wakipora bidhaa katika duka linalomilikiwa na raia wa kigeni kutoka nchi za Afrika

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vitendo vya ghasia dhidi ya wageni nchini Afrika Kusini vinavyoenda sambamba na mashumbulizi dhidi ya raia wa kigeni pamoja na uharibifu wa mali. Guterres ametambua na kuunga mkono kauli ya Rais Cyril Ramaphosa ya kulaani vikali vitendo hivyo na wito wake wa kutaka kuimarishwa uwajibikaji kwa mujibu wa maadili ya Afrika Kusini yaliyoainishwa kwenye katiba.