Mamia ya raia wa Nigeria wanaoishi Afrika Kusini kurejeshwa nyumbani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55916-mamia_ya_raia_wa_nigeria_wanaoishi_afrika_kusini_kurejeshwa_nyumbani
Serikali ya Nigeria inatazamiwa kuanza kuwarejesha nyumbani mamia ya raia wake wanaoishi nchini Afrika Kusini, kufuatia wimbi la ghasia na mashambulizi yaliowalenga wageni katika nchi hizo mbili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 10, 2019 03:11 UTC
  • Mamia ya raia wa Nigeria wanaoishi Afrika Kusini kurejeshwa nyumbani

Serikali ya Nigeria inatazamiwa kuanza kuwarejesha nyumbani mamia ya raia wake wanaoishi nchini Afrika Kusini, kufuatia wimbi la ghasia na mashambulizi yaliowalenga wageni katika nchi hizo mbili.

Kwa mujibu wa Godwin Adama, balozi mdogo wa Nigeria mjini Johannesburg, ndege mbili zitabeba kundi la kwanza la raia wa Nigeria kesho Jumatano, ambao ni kati ya Wanigeria 600 watakaorejeshwa nchini katika mpango huo. 

Wakati huo huo,  Abike Dabiri, Mkuu wa Kamisheni ya Wanigeria Wanaoishi Nje ya Nchi amesema serikali ya Abuja haitatoa msaada wa kifedha kwa raia wake watakaorejeshwa nyumbani wakitokea Afrika Kusini.

Badala yake amesisitiza kuwa Nigeria itaendelea kuishinikiza Afrika Kusini iwape fidia raia wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika waliolazimika kuacha kazi na biashara zao nchini Afrika Kusini. Mashambulizi dhidi ya raia wa kigeni huko Afrika Kusini yameibua hasira kote barani Afrika ambapo maduka yanayomilikiwa na mashirika ya Afrika Kusini yameporwa nchini Nigeria.

Waafrika Kusini wakipora maduka ya wageni

Hii ni katika hali ambayo, Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria anatazamiwa kutembelea Afrika Kusini mwezi ujao kujaribu kuboresha uhusiano uliovurugika wa nchi mbili kufuatia wimbi hilo la ghasia.

Wiki iliyopita, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini alisema watu wasipungua 10 wameuawa katika ghasia na hujuma dhidi ya raia wa kigeni nchini humo.