Sep 19, 2019 07:40 UTC
  • Kiongozi wa wasi wa FDLR kutoka Rwanda auawa huko Congo DR

Kiongozi wa waasi wa Kihutu kutoka Rwanda aliyekuwa akisakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kwa tuhuma za kufanya jinai za kivita ameuawa kwa kipigwa risasi na askari wa jeshi la Congo.

Msemaji wa Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Jenerali Leon-Richard Kasonga amesema kuwa Sylvestre Mudacumura aliyekuwa kamanda wa genge la waasi wa Rwanda la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR), aliuawa Jumanne iliyopita katika jimbo la Kivu Kaskazini, umbali wa kilomita 60 kutoka katika mji wa Goma.

Mudacumura alikuwa akisakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai yenye makao yake makuu huko The Hague nchini Uholanzi kwa kuhusika na uhalifu kadhaa ikiwa ni pamoja na kubaka, kutesa na kupora mali za raia.

Kundi la FDLR liliundwa na wakimbizi wa Kihutu huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watustsi katika nchi jirani ya Rwanda.

Kundi la waasi wa FDLR linafanya ukatili na mauaji mashariki mwa Congo DR.

Kundi hilo linalaumiwa kwa kufanya ukatili na mauaji ya kutisha dhidi ya raia wa maeneo ya mashariki mwa Congo.   

Tags