30 wapoteza maisha katika maporomoko ya udongo mgodini Chad
Makumi ya wachimba migodi wamefariki dunia baada ya kuporomokewa na udongo kwenye mgodi haramu wa dhahabu nchini Chad.
Hayo yalisemwa jana Alkhamisi na Mahamat Sala, Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo katika mahojiano na shirika la habari la Reuters na kuongeza kuwa, maporomoko hayo yalitokea Jumanne katika eneo la Tibesti, mpakani na Libya.
Amesema watu 30 wamethibitishwa kuaga dunia katika mkasa huo na kwamba, yumkini kuna wahanga wengine wa ajali hiyo ambao wangali wamefunikwa kwenye maporomoko hayo.
Eneo la Tibesti limeshuhudia ongezeko la uchimbaji madini kinyume cha sheria katika miaka ya hivi karibuni, ambao aghalabu unafanywa na wahajiri kutoka Sudan wanaotaka pesa za haraka kwa ajili ya kwenda kutafuta maisha barani Ulaya.
Mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu, watu 43 waliaga dunia katika maporomoko mengine yaliyotokea kwenye mgodi wa shaba nyekundu na kobalti kusini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mgodi huo unasimamiwa na kampuni ya Glencore yenye makao makuu yake mjini Baar nchini Uswisi.
Aghalabu ya madini hususan ya dhahabu na almasi yanayochimbwa Kongo DR na Chad miongoni mwa nchi nyingine za Afrika, husafirishwa kimagendo katika nchi za Ulaya na Uarabuni.