UN yakaribisha kuongezwa muda wa kipindi cha mpito Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57217-un_yakaribisha_kuongezwa_muda_wa_kipindi_cha_mpito_sudan_kusini
Umoja wa Mataifa umekaribisha uamuzi wa Shirika la Kiserikali la Ustawi wa nchi za Mashariki mwa Afrika (IGAD) wa kurefusha kwa siku 100 kipindi cha mpito nchini Sudan Kusini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 12, 2019 04:31 UTC
  • UN yakaribisha kuongezwa muda wa kipindi cha mpito Sudan Kusini

Umoja wa Mataifa umekaribisha uamuzi wa Shirika la Kiserikali la Ustawi wa nchi za Mashariki mwa Afrika (IGAD) wa kurefusha kwa siku 100 kipindi cha mpito nchini Sudan Kusini.

IGAD ilichukua uamuzi huo baada ya mazungumzo kati ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na hasimu wake Riek Machar yaliyofanyika siku chache zilizopita jijini Kampala chini ya upatanishi wa Rais Yoweri Museveni, kumalizika bila pande mbili kulegeza misimamo na kuonekana kuwa tayari kwa uundaji wa serikali hiyo.

Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema Antonio Guterres amezitaka pande hasimu za Sudan Kusini zitumie muda huo kupatia ufumbuzi utesi na mgogoro uliopo, ili kuhakikisha kuwa serikali hiyo moya ya umoja wa kitaifa inaundwa kufikia mwezi Februari mwaka ujao 2020. 

Mwezi Mei mwaka huu pande mbili hasimu za Sudan Kusini zilitia saini makubaliano ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa katika kipindi cha miezi sita ijayo na kuunda serikali ya mpito hadi kufikia tarehe 12 Novemba (leo Jumanne).

Rais Kiir (kushoto) na Riek Machar walipofikia makubaliano ya kwanza ya amani miaka 4 iliyopita

Mapatano ya amani kati ya serikali ya Sudan Kusini na makundi ya waasi yamekuwa yakisainiwa kila uchao, lakini kila mara yamekuwa yakikiukwa.

Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya ndani Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kuipindua serikali yake.