UN: Sudan Kusini yasajili kikosi kipya cha wapiganaji kinyume na makubaliano
Umoja wa Mataifa umesema Idara ya Usalama wa Taifa ya Sudan Kusini imeunda kikosi kipya chenye wapiganaji 10,000 kinyume na makubaliano ya amani.
Ripoti iliyotolewa na timu ya wataalamu wanaofuatilia masuala ya vikwazo dhidi ya Sudan Kusini ya Umoja wa Mataifa imefichua kuwa, kikosi hicho kipya kinajumuisha hata watoto ambao aghalabu yao wamesajiliwa kwa nguvu.
Ripoti hiyo ya UN imesema wapiganaji hao wanapatikana katika ngome za kisiasa na maeneo ya kikabila ambayo Rais Salva Kiir wa nchi hiyo ana ushawishi mkubwa na kukubalika.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, kikosi hicho kinapokea amri moja kwa moja kutoka kwa Idara ya Usalama wa Taifa ya Sudan Kusini, na kwamba kimeundwa baada ya Rais Kiir na idara hiyo ya usalama kuwashawishi wazee wa kabila la Dinka kuhusu umuhimu wa kusajili wapiganaji watiifu kwa Kiir haswa katika jimbo la Mto Yei.
UN inasisitiza kuwa, usajili huo wa kikosi kipya cha wapiganaji watiifu kwa Salva Kiir unakiuka vipengee vya makubaliano ya amani yanayotaka kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa.
Hii ni katika hali ambayo, Umoja wa Afrika umewapa mahasimu wa kisiasa wa Sudan Kusini Rais Salva Kiir na kiongozi wa upinzani, Riek Machar nafasi ya mwisho ya kuunda serikali ya pamoja, baada ya kushindwa kufanya hivyo tarehe 12 mwezi Novemba. Rais Kiir na Machar, walikubaliana kuunda serikali hiyo ndani ya siku 100 zijazo, baada ya kukutana nchini Uganda.