Marasimu ya miaka 41 ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yafanyika Senegal
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59141-marasimu_ya_miaka_41_ya_ushindi_wa_mapinduzi_ya_kiislamu_yafanyika_senegal
Marasimu ya kuadhimisha mwaka wa 41 wa Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamefanyika nchini Senegal.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 14, 2020 03:59 UTC
  • Marasimu ya miaka 41 ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yafanyika Senegal

Marasimu ya kuadhimisha mwaka wa 41 wa Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamefanyika nchini Senegal.

Shirika la habari la Fars News limeripoti hayo na kuongeza kuwa, marasimu hayo yamehudhuriwa na mabalozi, maafisa wa kidiplomasia, waandishi wa habari, viongozi wa kidini wa Senegal pamoja na Wairani wanaoishi katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Mohammad Reza Dehshiri, Balozi wa Iran nchini Senegal ambaye ni mmoja wa washiriki wa marasimu hayo ameashiria kuhusu nafasi isiyo na mithili ya Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Qods cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH aliyeuawa shahidi mapema mwaka huu katika shambulizia la kigaidi na Marekani nchini Iraq, ambaye alisabilia maisha yake katika kupambana na ugaidi.

Aidha amekosoa sera za uhasama na za upande mmoja za Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kueleza bayana kuwa, maafisa wa Washington hawaheshimu kanuni na sheria za kimataifa.

Balozi wa Iran nchini Senegal kadhalika amegusia kuhusu hatua ilizopiga Jamhuri ya Kiislamu katika nyuga za sayansi na teknolojia, katika hotuba yake kwenye marasimu hayo ya maadhimisho ya mwaka wa 41 wa Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Senegal.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alipoitembelea Senegal

Maafisa wa serikali ya Senegal walioshiriki marasimu hayo wamesisitizia umuhimu wa kuimarishwa uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hiyo ya Kiafrika na Iran katika nyuga za viwanda na nishati.

Maadhimisho ya mwaka huu ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yamesadifiana na arubaini ya Jenerali Soleimani, kamanda wa Iran aliyeuliwa shahidi akiwa pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Mkuu wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq cha Hashd al Sha'abi pamoja na wanajihadi wengine wanane katika shambulio la kigaidi la wanajeshi wa Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad Januari 3.  

Matembezi, marasimu na vikao vya kuadhimisha matukio hayo mawili ya kihistoria vimefanyika katika pembe mbali mbali za Iran.