Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya ajiuzulu
Ghassan Salamé, mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya ametangaza kujiuzulu wadhifa huo, huku mgogoro wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ukishtadi.
Stephane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema Antonio Guterres amepokea barua ya kujiuzulu Salame, kutokana na sababu za kiafya.
Salame ambaye ni raia wa Lebanon aliteuliwa kuwa mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa UN katika masuala ya Libya mnamo Juni mwaka 2017.
Mwanadiplomasia huyo wa UN ametangaza kujiuzulu ikiwa ni siku chache baada ya kusema kuwa, pande mbili hasimu nchini Libya zimeafiki mpango wa kuundwa Kamati ya Pamoja ya Kijeshi chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa, kwa minajili ya kuzipatia ufumbuzi hitilafu zilizopo baina ya pande hizo.
Mgogoro wa Libya ambao ulianza tokea mwaka 2011 baada ya kupinduliwa kanali Muammar Gaddafi, ulishadidi na kuwa mkubwa baada ya janerali muasi Khalifa Haftar kuanzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli mwezi Aprili mwaka jana.
Mashambulizi hayo yameua na kujeruhi maelfu ya watu katika mji mkuu huo wa Libya, mbali na kusababisha malaki ya wengine kukimbia makazi yao.