Kuendelea uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i60156-kuendelea_uingiliaji_wa_marekani_katika_masuala_ya_ndani_ya_sudan
Uingiliaji wa Marekani katika nchi za Afrika kwa njia ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja, ungali unaendelea.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 04, 2020 02:43 UTC
  • Kuendelea uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Sudan

Uingiliaji wa Marekani katika nchi za Afrika kwa njia ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja, ungali unaendelea.

Katika uwanja huo Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani na katika mazugumzo ya simu na Abdalla Hamdok, Waziri Mkuu wa Sudan amesisitizia uungaji mkono wa nchi yake kwa serikali ya mpito ya nchi hiyo na kile kinachotajwa kuwa juhudi za Washington kwa ajili ya kurejesha usalama na uthabiti ndani ya taifa hilo la Kiafrika. Katika matamshi ya uingiliaji huo, Pompeo ametaka kuharakishwa mwenendo wa kuundwa baraza la kutunga sheria (yaani bunge) katika kipindi cha mpito sambamba na kuteuliwa magavana wasio wa kijeshi. Kuondolewa jina la Sudan katika orodha ya ugaidi, makabiliano ya virusi vya Corona na kuongezwa ushirikiano wa nchi mbili katika uwanja huo, ni sehemu nyingine iliyotawala mazungumzo ya Pompeo na Hamdok. Sudan inahesabika kuwa nchi muhimu kwa Marekani na washirika wake wakuu yaani utawala haramu wa Israel na Saudia. Hata kama Omar Hassan Al-Bashir, rais wa zamani wa nchi hiyo katika miaka ya hivi karibuni alifanya juhudi kubwa za kubadili msimamo na siasa zake kwa matarajio ya kupata uungaji mkono wa kifedha na kisiasa, kupitia kutekeleza matakwa ya Washington na washirika wake kama vile kujiunga serikali ya Khartoum katika muungano vamizi wa kijeshi wa Saudia katika vita vyake nchini Yemen, lakini pamoja na hayo Al-Bashir hakuweza kubadili msimamo wa raia wa nchi yake. Baada ya kuondolewa madarakani rais huyo wa zamani, Abdalla Hamdok aliteuliwa kuwa waziri mkuu mpya wa Sudan na tangu wakati huo amekuwa akiongoza serikali ya mpito ya nchi hiyo.

Abdalla Hamdok na Mike Pompeo

Hamdok kama alivyokuwa mtangulizi wake, ameelekeza siasa zake kwenye kupanua na kustawisha uhusiano na Washington na washirika wake na hasa anataka kuondolewa jina la Sudan katika orodha ya nchi zinazodaiwa na Marekani kuunga mkono ugaidi. Serikali ya Marekani iliweka jina la Sudan katika orodha yake ya nchi zinazodaiwa kuunga mkono ugaidi mwaka 1997 kufuatia mapigano ya eneo la Darfur, ambapo pia iliiwekea vikwazo. Aidha tarehe 6 Oktoba 2017 serikali ya Rais Donald Trump iliifutia Sudan vikwazo vya kiuchumi na marufuku ya kibiashara iliyokuwa imeiwekea nchi hiyo, lakini pamoja na hayo bado miamala ya kifedha ya pande mbili bado haifanyiki, na hivyo nchi nyingi za Ulaya zinasubiri kuondolewa rasmi serikali ya Khartoum katika orodha ya kigaidi. Ni kwa ajili hiyo, ndio maana serikali mpya ya Sudan inafanya juhudi za kuikinaisha Washington ili ibadili mtazamo wake kwa kuiondoa katika orodha ya waungaji mkono wa ugaidi. Vikao na mazungumzo na viongozi wa Marekani na pia wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel sambamba na kuruhusu ndege za Israel kutumia anga ya Sudan na kuendelea kushiriki katika muungano vamizi wa kijeshi wa Saudia dhidi ya taifa madhlumu la Yemen, ni sehemu ya juhudi za viongozi wa sasa wa Sudan kwa ajili ya kuvutia mtazamo na uzingatiaji wa Washington. Hii ni katika hali ambayo kuna ukosoaji mwingi kuhusu utendajikazi wa serikali ya sasa ya Khartoum. Kwa mtazamo wa Wasudan, migogoro inayoikumba nchi hiyo haisababishwi na kukatwa uhusiano wa Sudan na utawala haramu wa Kizayuni au kutoboreka uhusiano na utawaka huo ghasibu, bali ufisadi, kukosekana serikali imara na stahiki pamoja na utawala wa kijeshi ndiyo mambo yaliyoitumbukiza nchi hiyo katika hali ya sasa.

Kujipendekeza kwa watawala wa Kizayuni, ni aina nyingine ya hiana kwa taifa la Sudan

Kuhusiana na suala hilo, Abir Al-Majmar, mtaalamu wa masuala ya siasa anasema: "Hasira na kutoridhishwa na hatua za serikali ya mpito, ni hisia zilizoenea katika jamii nzima ya Sudan. Wananchi wanaitaka serikali sambamba na kurekebisha makosa yake, ifanye juhudi za kubadili hali ya hapo kabla, na kushughulikia masuala muhimu ya nchi na hasa suala la kuhitimisha vita vya Yemen." Licha ya matakwa ya Wasudan na sisitizo lao la kulindwa matukufu ya nchi, lakini viongozi wa nchi hiyo wanaona kuwa njia pekee ya kutatua matatizo ya sasa ni kurejesha uhusiano na Marekani. Hii ni katika hali ambayo kugawanywa nchi hiyo na kuundwa taifa linaloitwa Sudan Kusini, kuporwa maliasili za Sudan na pia kuishawishi nchi hiyo iendelee kushiriki kijeshi katika vita vya Yemen, ni mambo yalifanyika kwa lengo la kutafuta ridhaa ya Washington na waitifaki wake. Inaonekana kwamba viongozi wa Washington bado wanaendelea kutumia mazingira ya sasa ya Sudan kwa ajili ya kujinufaisha wao na washirika wao. Kuhusiana na suala hilo, Bashir Adam Rahma, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi cha Sudan, amesema: “Iwapo tutasimamia vizuri masuala ya ndani, hakuna mtu atakayemwomba yeyote kutuondolea vikwazo vya Marekani. Kutegemea dhahabu kunaweza kututatulia matatizo yetu ya kiuchumi. Iwapo mambo yatasimamiwa vizuri, Sudan itaweza kuingiza kiasi kinachofikia dola bilioni 10 kwa mwaka.” Hivi sasa kwa mara nyingine viongozi wa Marekani kwa kutoa ahadi za kuiondoa Sudan katika orodha ya nchi zinazodaiwa kuunga mkono ugaidi, wanakusudia kuendeleza uingiliaji wao katika nchi hiyo ya Kiafrika kwa lengo la kulinda maslahi yao na ya washirika wao, suala ambalo akthari ya vyama na raia wa Sudan wanalipinga vikali.