Mvua, mafuriko na maporomoko ya ardhi yasababisha maafa Kenya
Kwa akali watu 12 wamepoteza maisha kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika baadhi ya maeneo ya Kenya.
Mshirikishi wa eneo la Bonde la Ufa, George Natembeya amesema, watu sita wakiwemo maafisa wawili wa polisi, wamefariki katika maporomoko ya udongo yaliyotokea kwenye mpaka wa kaunti za Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet kufuatia mvua kubwa zilizonyesha usiku wa Jumamosi.
Kadhalika watu wengine sita wameaga dunia katika eneo la Chesogon kauti ya Pokot Magharibi kutokana na mafuriko, mbali na mamia ya familia kuachwa bila makazi.
Habari zaidi zinasema kuwa, kuna watu kadhaa ambao hawajulikani walipo kutokana na mafuriko hayo, huku timu za uokoaji zikiendelea kuwatafuta kando ya Mto Chesogon. Aidha wakazi wa eneo hilo wametakiwa kuhamia nyanda za juu na kwenye maeneo salama ili kuepusha maafa zaidi kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika eneo hilo.

Hii ni katika hali ambayo, kwa akali watu 23 wameaga dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa kutokana na mafuriko huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kufuatia mvua kali zilizonyesha siku za Ijumaa na Jumamosi.
Uongozi wa mkoa wa Kivu Kusini umesema watu elfu 80 wameachwa bila makazi kufuatia janga hilo la kimaumbile na hivyo kuifanya serikali ya mji wa Kivu Kusini kuomba msaada.