Asasi ya kiraia yakosoa hali mbaya ya jela za Misri
(last modified Thu, 30 Apr 2020 12:45:34 GMT )
Apr 30, 2020 12:45 UTC
  • Asasi ya kiraia yakosoa hali mbaya ya jela za Misri

Kwa mujibu wa kanali moja ya Kiarabu inayotoa taarifa kuhusu haki za binaadamu, ukandamizaji na virusi vya Corona vinawahangaisha wafungwa na mahabusu katika jela za Misri na kuwasumbua.

Kanali hiyo inayojiita Kanali ya Habari za Haki za Binadamu ambayo ni taasisi ya kiraia na iliyo na makao yake Cairo, mji mkuu wa Misri, imetoa taarifa ikisema kuwa, virusi vya Corona 'ni njia ya kuwatesa wafungwa na mahabusu' nchini humo. Taarifa hiyo inaeleza kwamba, badala ya kuwaachilia huru wafungwa na watu wanaoshikiliwa kama njia mojawapo ya kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona, ugonjwa huo umegeuka na kuwa moja ya njia za ziada za utesaji ambapo wanazuiliwa kukutana na jamaa zao. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hali ya wafungwa wa Misri ni mbaya sana ambapo wananyimwa haki zao za msingi. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, serikali na taasisi zenye mafungamano na serikali hiyo, zimeongeza dhulma dhidi ya wafungwa ambapo huwa zinawaongezea vifungo kwenye karatasi tu bila ya wao kuwepo mahakamani wala mawakili wao.

Rais Abdel-Fattah El-Sisi wa Misri anayekosolewa kila mara kwa ukandamizaji

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri na kwa kisingizio cha kulinda usalama na afya za wanaowatembelea wafungwa, ilipiga marufuku wageni kuwatembelea wafungwa tokea tarehe 10 Machi iliyopita.  Kwa ajili hiyo kanali hiyo imetoa pendekezo kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri kuacha kukiuka haki za wafungwa kwa kisingizio cha usalama kwa kuwa jambo hilo kimsingi ni ukiukaji wa haki zao.

Tags