Mafuriko yaua watu 260 Kenya, Rwanda na Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i60849
Kwa akali watu 260 wamepoteza maisha kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika nchi za Afrika Mashariki za Kenya, Rwanda na Somalia.
(last modified 2025-07-22T07:00:06+00:00 )
May 08, 2020 08:18 UTC
  • Mafuriko yaua watu 260 Kenya, Rwanda na Somalia

Kwa akali watu 260 wamepoteza maisha kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika nchi za Afrika Mashariki za Kenya, Rwanda na Somalia.

Kenya ndiyo nchi iliyoaathirika zaidi na majanga hayo ambapo hadi sasa watu 194 wameaga dunia kwenye mafuriko hayo ambayo pia yameharibu zaidi ya ekari elfu 8 za mashamba ya kilimo.

Kadhalika mafuriko hayo yameua watu 55 nchini Rwanda, ambapo akthari yao wameaga dunia katika maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mafuriko hayo katika maeneo yenye milima mingi ya kaskazini magharibi mwa nchi.

Habari zaidi zinasema kuwa, watu 16 wamefariki dunia kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini Somalia, huku wagonjwa 200 wakikwama hospitalini kutokana na kuzingirwa na maji ya mafuriko nchini Uganda.

Mafuriko Somalia

Mwezi uliopita, makumi ya watu waliaga dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa kutokana na mafuriko katika mkoa wa Kivu Kusini huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, huku wengine zaidi ya elfu 80 wakichwa bila makazi kufuatia janga hilo la kimaumbile.

Mwishoni mwa mwaka jana, majanga yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha katika nchi za Afrika Mashariki yalipelekea watu 250 kuaga dunia, mbali na wengine zaidi ya milioni tatu kuathirika na majanga hayo kwa njia moja au nyingine.