May 21, 2020 02:35 UTC
  • Askari 19 wa Niger na Nigeria wauawa katika mashambulizi ya Boko Haram

Wanajeshi wasiopungua 12 wa Niger wameuawa katika shambulizi la kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram katika eneo la Diffa, kusini mashariki mwa nchi.

Wizara ya Ulinzi ya Niger ilitangaza hayo Jumanne na kuongeza kuwa, wanajeshi hao wameuawa baada ya kambi yao ya Blabrine kushambuliwa na wananchama wa kundi la kigaidi la Boko Haram karibu na mji wa Diffa, kusini mashariki mwa nchi hiyo.

Taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Niger imebainisha kuwa, wanajeshi wengine kumi wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika wamejeruhiwa katika shambulio hilo la wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram.

Shambulizi hilo linaonekana kuwa la ulipizaji kisasi haswa kwa kuzingatia kuwa, limejiri siku chache baada ya Wizara ya Ulinzi ya Niger kutangaza habari ya kuuawa wanachama 75 wa kundi hilo la kigaidi katika operesheni mbili za jeshi la nchi hiyo huko kusini mashariki mwa nchi.

Wanajeshi wa Nigeria katika operesheni

Katika hatua nyingine, askari saba wa jeshi la Nigeria wameuawa katika mashambulizi ya kundi la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram kaskazini mashariki mwa nchi. Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, wanajeshi hao wameuawa baada ya wananchama wa genge hilo kushambulia mji wa Dapchi na kijiji cha Maza, kaskazini mashariki mwa Nigeria. 

Haya yanajiri masaa machache baada ya Jeshi la Nigeria kutangaza kuwa, limewaua wanachama 20 wa kundi hilo la kigaidi katika jimbo la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo la Borno.

Tags