Kurejea Misri katika Bunge la Afrika
Baada ya miaka kadhaa ya kuwa nje ya Bunge la Afrika, kwa mara nyingine tena Misri imerejea kwenye bunge hilo. Kuhusu suala hilo Ali Abdel Aal, spika wa bunge la Misri ameongoza ujumbe wa nchi yake katika kikao cha Bunge la Afrika huko Johannesburg Afrika Kusini.
Ujumbe huo wa Misri uliapishwa katika sherehe rasmi zilizofanyika kwa mnasaba huo wa kurejea tena Misri kwenye Bunge la Umoja wa Afrika AU. Ripoti zinasema vikao vya bunge hilo vitaendelea hadi Mei 13 mwaka huu. Wawakilishi wa Misri wamesema kuwa vikao vya bunge hilo vitasaidia kuimarishwa uhusiano wa nchi yao na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Afrika. Bunge la Afrika ni taasisi ya utungaji sheria ya Umoja wa Afrika ambayo iliasisiwa mwezi Machi 2004 kwa kutiwa saini hati ya kuasisiwa kwake na nchi 36 wanachama wa umoja huo. Bunge hilo lina wabunge 265 ambao huchaguliwa na mabunge ya kitaifa ya nchi wanachama. Makao makuu ya kudumu ya bunge hilo yako Afrika Kusini. Uchaguzi wa mwisho wa bunge la Misri ulifanyika miezi michache baada ya kuangushwa utawala wa dikteta Husni Mubarak, rais wa zamani wa nchi hiyo hapo mwaka 2011 ambapo chama cha Ikhwanul Muslimeen kiliibuka na ushindi kwa kupata karibu nusu ya viti vyote vya bunge. Hata hivyo bunge hilo lilivunjwa mwaka 2012 kwa amri ya mahakama, siku chache tu kabla ya Rais Muhammad Mursi aliyechaguliwa kidemokrasi na wananchi kutwaa madaraka. Misri iliendelea kuwa bila ya bunge tokea wakati huo hadi hatimaye uchaguzi mkuu ulipofanyika mwaka uliopita. Katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo iliyofanyika tarehe 18 na 19 za mwezi Oktoba mwaka uliopita, ni asilimia 26.6 tu ya watu waliotimiza masharti ya kupiga kura ndio walioshiriki kwenye uchaguzi huo. Idadi hiyo ilipungua hata zaidi katika duru ya pili ya uchaguzi ambapo ni asilimia 21.7 tu ya raia ndio walioshiriki kwenye uchaguzi. Wagombea wa Ikhwanul Muslimeen ambacho ni chama kikuu cha upinzani nchini Misri walizuiwa kushiriki kwenye uchaguzi huo. Vyama vya kisoshalisti na kiliberali ambavyo awali vilikuwa vimetangaza nia yao ya kushiriki kwenye uchaguzi, hatimaye viliususia. Wakosoaji walitilia shaka uhalali wa uchaguzi mkuu huo kutokana na kuwa serikali ilitumia mkono wa chuma kuwakandamiza wapinzani wake. Bunge la Misri ambalo lina waungaji mkono wengi wa Rais Abbdulfattah as-Sisi wa nchi hiyo lina wabunge 568 wa kuchaguliwa na 28 wa kuteuliwa ambao huteuliwa moja kwa moja na Rais as-Sisi mwenyewe. Bunge hilo lina jukumu la kuchunguza na kupitisha miswada karibu 300 ambayo iliwasilishwa bungeni tokea mwaka 2014 na wakati wa kuingia madarakani as-Sisi na hata kabla ya hapo katika kipindi cha uongozi wa Adly Mansour, rais wa muda wa wakati huo wa Misri. Mswada muhimu zaidi kati ya hizo ni ule unaobana maandamano na malalamiko ya wapinzani mitaani, kubana uhuru wa kujieleza, wa magazeti na wakati huohuo kulipa jeshi la polisi uwezo mkubwa wa kukandamiza wapinzani wa serikali.