Jeshi la Ethiopia laua viongozi kadhaa wa TPLF eneo la Tigray
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i65659-jeshi_la_ethiopia_laua_viongozi_kadhaa_wa_tplf_eneo_la_tigray
Viongozi wanne wa Harakati ya Ukombozi ya Wananchi wa Tigray (TPLF) wameripotiwa kuuawa katika operesheni ya vikosi vya jeshi la Ethiopia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 09, 2021 02:40 UTC
  • Jeshi la Ethiopia laua viongozi kadhaa wa TPLF eneo la Tigray

Viongozi wanne wa Harakati ya Ukombozi ya Wananchi wa Tigray (TPLF) wameripotiwa kuuawa katika operesheni ya vikosi vya jeshi la Ethiopia.

Taarifa ya Jeshi la Ulinzi la Ethiopia imesema kuwa, mbali na viongozi wanne wa TPLF kuuawa, lakini wengine tisa wamejeruhiwa. Miongoni mwa viongozi wa TPLF waliouawa katika operesheni hiyo ya jeshi la Ethiopia ni Katibu Mkuu wa harakati hiyo, Sekoture Getachew na Daniel Assefa, mkuu za zamani wa hazina wa eneo la Tigray.

Aidha Zeray Asgedom, aliyekuwa mkuu wa Mamlaka ya Utangazi ya Ethiopia (EBA) na mwandishi wa habari aliyekuwa karibu na harakati hiyo Abebe Asgedom wameuliwa pia katika operesheni hiyo ya vikosi vya ulinzi vya Ethiopia.

Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Tesfaye Aylew, afisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Ulinzi la Ethiopia, wanachama wengine tisa wa Harakati ya Ukombozi ya Wananchi wa Tigray wametiiwa mbaroni katika operesheni hiyo.

Mwezi Novemba mwaka uliomalizika 2020, serikali ya Addis Ababa ilitoa waranti wa kutiwa mbaroni viongozi zaidi ya 60 wa TPLF, ingawaje habari kuhusu aliko mwenyekiti wa harakati hiyo, Debrestion Gebremichael na maafisa wengine wa ngazi za juu wa harakati hiyo haijulikani. 

Baadhi ya wapiganaji wa TPLF

Eneo la Tigray lililoko kaskazini ya Ethiopia limeshuhudia mapigano katika wiki za karibuni kati ya jeshi la nchi hiyo na vikosi vya Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray TPLF.

Serikali ya Addis Ababa, ambayo inaituhumu TPLF kuwa inataka kulitenganisha eneo la Tigray na ardhi ya Ethiopia, lilitangaza hivi karibuni kuwa vikosi vya jeshi vimeudhibiti mji wa Mekelle, makao makuu ya eneo hilo. Hata hivyo mapigano yanaripotiwa kuendelea mashariki mwa mji hu, makao makuu ya jimbo la Tigray.