Ethiopia yasema imeua wapiganaji 15 wa eneo la Tigray
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i65716-ethiopia_yasema_imeua_wapiganaji_15_wa_eneo_la_tigray
Jeshi la Ethiopia limetangaza habari ya kuua wanachama wengine 15 wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray TPLF, ambacho kilikuwa chama tawala katika eneo la Tigray, kaskazini mwa nchi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 12, 2021 03:36 UTC
  • Ethiopia yasema imeua wapiganaji 15 wa eneo la Tigray

Jeshi la Ethiopia limetangaza habari ya kuua wanachama wengine 15 wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray TPLF, ambacho kilikuwa chama tawala katika eneo la Tigray, kaskazini mwa nchi.

Hayo yametangazwa na Shirika la Utangazi la Ethiopia (EBC), likimnukuu Brigedia Jenerali wa Jeshi la Ulinzi la nchi hiyo. Eneo la Tigray limeshuhudia mapigano katika miezi ya karibuni kati ya jeshi la nchi hiyo na vikosi vya TPLF.

Kwa mujibu wa EBC,  mbali na viongozi 15 chama hicho tawala cha zamani katika eneo la Tigray kuuawa, lakini wengine wanane wametiwa mbaroni, akiwemo rais wa zamani wa eneo hilo, Abay Weldu na aliyekuwa makamu wake Abraham Tekeste.

Miongoni mwa wapiganaji wa eneo la Tigray waliouawa katika operesheni hiyo ya Jumapili ni Naibu Kamishna wa Polisi wa zamani wa eneo hilo.

Ijumaa iliyopita, jeshi la Ethiopia lilitangaza kuwa limemkamata mmoja wa waasisi wa Harakati ya Ukombozi ya Wananchi wa Tigray (TPLF), Sebhat Nega na kumhamishia katika mji mkuu, Addis Ababa.

Wapiganaji wa TPLF

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya viongozi wanne wa Harakati ya Ukombozi ya Wananchi wa Tigray kuripotiwa kuuawa katika operesheni ya vikosi vya jeshi la Ethiopia, mbali na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Mwezi Novemba mwaka uliomalizika 2020, serikali ya Addis Ababa ilitoa waranti wa kutiwa mbaroni viongozi zaidi ya 60 wa TPLF, ingawaje hadi sasa hakuna anayefahamu aliko mwenyekiti wa harakati hiyo, Debrestion Gebremichael.