Maelfu wakamatwa Afrika Kusini kwa kutovaa barakoa
Polisi ya Afrika Kusini imewatia mbaroni maelfu ya watu waliokutwa katika maeneo ya umma bila barakoa.
Katika kikao na waandishi wa habari jana Jumatano, Waziri wa Polisi wa Afrika Kusini, Bheki Cele alisema zaidi ya watu 7,000 wametiwa nguvu na maafisa usalama wa nchi hiyo kwa kutembea bila kuvaa barakoa katika maeneo ya umma, tokea mwishoni mwa mwezi uliopita wa Disemba hadi sasa.
Amesema zaidi ya watu 20,000 wamekamatwa tokea wakati huo hadi sasa kwa kukiuka maagizo mapya yaliyotangazwa na serikali kwa shabaha ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.
Aidha watu 830 wametia nguvuni kwa kuuza, kununua au kusafirisha pombe tokea Disemba 29 hadi sasa, kinyume na kanuni mpya zilizotangazwa za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.
Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Disemba, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini alitangaza sheria kali za kudhibiti msambao wa virusi vya corona, baada ya nchi hiyo kusajili kesi zaidi ya milioni moja ya ugonjwa wa Covid-19 kufikia sasa.
Mbali ya kupiga marufuku mikusanyiko ya aina yoyote ile ya ndani na nje ya majumba na kurejeshwa agizo la kutotoka nje kuanzia saa tatu usiku hadi 12 alfajiri, lakini pia alionya kuwa watakaotembea bila barakoa katika maeneo ya umma watapigwa faini au kufungwa jela kwa muda usiopungua miezi sita au yote mawili.
Nchi hiyo imerekodi zaidi ya kesi milioni 1.2 za maambukizi ya corona kufikia jana na vifo 34,000, na hivyo kuwa nchi ya Afrika iliyoandikisha kesi na vifo vingi zaidi vya maradhi hayo ya kuambukiza.
Inaaminika kuwa, spishi mpya ya kirusi cha corona iliyoripotiwa mara ya kwanza nchini Uingereza na inayofamika kwa kitaalamu kama 501.V2 ndiyo sababu ya ongezeko hilo la kutisha la maambukizi ya maradhi hayo nchini Afrika Kusini ndani ya siku chache zilizopita.