Rais wa Afrika Kusini atangaza juhudi za kufufua uchumi nchini humo
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ametangaza habari za juhudi kubwa zinazofanywa na serikali yake za kufufua uchumi wa nchi hiyo ulioathiriwa vibaya na maambukizi ya kirusi hatari cha corona.
Mwandishi wa IRIB amemnukuu Rais Ramaphosa akisema hayo katika hotuba yake bungeni na kusisitiza kuwa, kipaumbele cha serikali yake kwa ajili ya mwaka huu wa 2021 ni kupambana na kirusi cha corona, kufufua uchumi na kupiga vita ufisadi wa kifedha uliokithiri nchini humo.
Ramaphosa amezungumzia pia mdororo wa kiuchumi na kupanda idadi ya watu wasio na ajira nchini Afrika Kusini kutokana na wimbi la ugonjwa wa COVID-19 na kusema kuwa, pato la ndani ya nchi katika kipindi cha miezi mitatu ya mwisho ya mwaka 2099 na 2020 lilipungua kwa asilimia 6 huku kiwango cha ukosefu wa ajira kikipanda kwa zaidi ya asilimia 30 nchini humo ndani ya kipindi hicho.
Baada ya Nigeria, Afrika Kusini ni ya pili kwa kuwa na uchumi mkubwa barani Afrika ikifuatiwa na Misri na Algeria.
Afrika Kusini inaongoza barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa na vifo vinavyotokana na ugonjwa wa COVID-19. Hadi jana (Jumamosi) usiku, Afrika Kusini ilikuwa imeshasajili wagonjwa 1,487,681 wa corona huku vifo vya watu waliokumbwa na ugonjwa huo vikifikia 47,670 nchini humo hadi jana usiku.
Kuzorota na kusambaratika uchumi na kupotea ajira ni miongoni mwa madhara makubwa ya ugonjwa wa COVID-19 katika mataifa ya dunia.