Serikali ya mpito ya Libya yafanya kikao chake cha kwanza tangu kuchaguliwa
Ofisi ya habari ya waziri mkuu wa serikali ya mpito ya Libya imetangaza kuwa kikao cha kwanza cha serikali hiyo kimefanyika baada ya wajumbe wake kuchaguliwa kupitia baraza la mazungumzo lililofanyika mjini Geneva, Uswisi.
Ofisi hiyo ya waziri mkuu wa serikali ya mpito wa Libya imeeleza kwamba, kikao hicho cha kwanza cha serikali hiyo kilifanyika jana Jumapili kwa kuhudhuriwa na waziri mkuuu Abdulhamid al-Dabaiba, mkuu wa baraza la urais Mohamed Yunus al-Menfi, pamoja na Abdullah Hussein Al Lafi na Musa Al Koni wajumbel wawili wa baraza hilo.
Katika kikao hicho, mkuu wa baraza la uongozi Mohamed Yunus al-Menfi amesisitiza kuwa, njia ya pwani inayounganisha miji ya Libya ya Sirte na Misrata itafunguliwa tena hivi karibuni na akaongeza kwamba, hatua hiyo ni miongoni mwa vipaumbele vya serikali ya mpito baada ya kupigiwa kura ya kuwa na imani nayo.
Aidha mkuu huyo wa baraza la uongozi la Libya ameitaka kamati ya kijeshi kuhakikisha usalama wa kikao cha bunge baada ya serikali ya mpito kupigiwa kura ya imani huko mjini Sirte.
Baada ya kupigwa kura katika kikao cha baraza la mazungumzo ya Libya kilichofanyika mjini Geneva chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa, Abdulhamid al-Dabaiba alichaguliwa waziri mkuu, Mohamed Yunus al-Menfi alichaguliwa mkuu wa baraza la urais na Musa Al Koni na Abdullah Hussein Al Lafi walichaguliwa kuwa wajumbe wawili wa baraza hilo.
Shakhsia hao walioshinda katika zoezi hilo la upigaji kura lililofanyika katika mazungumzo ya Geneva, watabeba jukumu la kuiongoza Libya kwa muda, hadi uchaguzi wa rais na bunge ambao umepangwa kufanyika Septemba 24 mwaka huu.../