Wabunge Libya wakutana kujadili baraza la mawaziri
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i67662-wabunge_libya_wakutana_kujadili_baraza_la_mawaziri
Wabunge wa pande hasimu nchini Libya wanakutana katika mji wa kistratijia wa Sirte kwa ajili ya kujadiliana kuhusu serikali ya Umoja iliyopendekezwa na Waziri Mkuu Abdul Hamid Dbeibah.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 08, 2021 11:26 UTC
  • Wabunge Libya wakutana kujadili baraza la mawaziri

Wabunge wa pande hasimu nchini Libya wanakutana katika mji wa kistratijia wa Sirte kwa ajili ya kujadiliana kuhusu serikali ya Umoja iliyopendekezwa na Waziri Mkuu Abdul Hamid Dbeibah.

Msemaji wa bunge Abdullah Belhaq amesema kuwa bado haijabainika wazi ni wabunge wangapi kati ya 200 waliochaguliwa mnamo mwaka 2014 watakaohudhuria kikao hicho ambacho kinaanza leo Jumatatu.

Baadhi ya wabunge tayari wamefariki, wengine wamejiuzulu na baadhi wamesema watasusia mkutano huo. Bunge linakutana kujadili litakavyoipa imani serikali iliyotangazwa na Abdulhamid Dbeibeh aliyeteuliwa kama waziri mkuu mwezi uliopita kupitia mazungumzo ya kisiasa yaliyoandaliwa mjini Geneva nchini Uswisi na Umoja wa Mataifa. Chini ya mchakato huo, serikali yake inatarajiwa tu kusimamia mipangalio ya uchaguzi uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu na baadaye kuwachia mamlaka viongozi watakaochaguliwa.

Abdulhamid Dbeibeh

Nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ambayo ni mzalishaji mkubwa wa mafuta imekuwa katika hali ya mchafukoge tangu mwaka 2011; pale muungano wa kijeshi wa Nato ulipoanzisha mashambulizi dhidi ya dikteta wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi.