Serikali ya muda ya Umoja wa Kitaifa Libya yaapishwa
Serikali ya muda ya Umoja wa kitaifa ya Libya iliapishwa jana Jumatatu na kuanza rasmi shughuli zake.
Sherehe za kuapishwa mawaziri wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya inayoongozwa na Waziri Mkuu Abdul-Hamid Dbeibah ilihudhuriwa na mabalozi na wawakilishi wa nchi mbalimbali walioko nchini humo.
Hata hivyo kutokana na kuwa, hadi sasa Walibya wameshindwa kuafikiana kuhusu mtu anayepaswa kushika wadhifa wa wizara nyeti ya Mambo ya Ndani, wizara hiyo itaongozwa na Waziri Mkuu mwenyewe.
Jumatano iliyopita, Bunge la Libya lililipigia kura Baraza la Mawaziri la nchi hiyo na kulipasisha kwa wingi mutlaki yaani kwa kura 132 kati ya 133 za wabunge waliohudhuria kikao hicho. Wananchi wa Libya wana matumaini kwamba uongozi mpya utamaliza miaka mingi ya mapigano ya silaha nchini mwao.
Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa, Waziri Mkuu Dbeibah na serikali yake wataongoza kipindi cha mpito hadi Desemba 24 mwaka huu wakati kutakapofanyika uchaguzi mkuu. Ofisi ya Waziri Mkuu imetangaza kuwa, mawaziri 27 wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa wanatoka katika maeneo ya mashariki, magharibi na kusini mwa nchi hiyo.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya imetangaza vipaumbele vyake kuwa ni kuimarisha huduma, kuleta umoja miongoni mwa taasisi za kiserikali na kuhitimisha kipindi cha mpito kwa kuitisha uchaguzi.