Kuapishwa Serikali ya Muda ya Libya, na changamoto zilizoko mbele yake
Hatimaye baada ya miezi kadhaa ya mivutano na kuainisha hatima ya siasa za Libya, Mawaziri wa Serikali ya Muda ya Umoja wa Kitaifa waliapishwa jana Jumatatu katika Bunge la nchi hiyo huko katika mji wa Tobruk.
Aguilla Saleh Issa, Spika wa Bunge la Libya amesema kuwa, kufanyika hafla ya kuapishwa mawaziri wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni hatua muhimu kwa ajili ya kurejesha demokrasia katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Spika wa Bunge la Libya ameitaka serikali hiyo kuanza kazi zake mara moja.
Kuanza kazi Serikali ya Muda ya Umoja wa Kitaifa ya Libya, ni kufunguliwa ukurasa mpya wa maisha ya kisiasa nchini humo. Libya imekuwa ikishuhudia vita, machafuko na mivutano ya kisiasa tangu mwaka 2011 baada ya kuondolewa madarakani kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi. Anga hiyo iliandaa uwanja wa uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo na kila moja kati ya madola hayo kutaka hisa katika uga wa kisiasa na kiuchumi wa nchi hiyo hususan maliasili na vyanzo vya utajiri vya Libya. Kushadidi hitilafu za ndani huko Libya na uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo katika miaka ya hivi karibuni kumeigeuza Libya na kuwa medani ya vita vya niaba vya madola ya kigeni kiasi kwamba, weledi wengi wa mambo walitoa indhari kuhusiana na kugawanyika nchi hiyo.
Kuzidi kuwa mbaya hali ya Libya baada ya kuenea virusi vya Corona sambamba na kupanuka wigo wa vita, ni mambo ambayo yaliwafanya wahusika wa ndani na waingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya Libya waridhie kufanya mazungumzo kwa ajili ya kuikwamua nchi hiyo kutoka katika kinamasi cha mgogoro wa sasa.
Mazungumzo ya Libya yalifanyika kwa kuhudhuriwa na wawakilishi wa makundi mbalimbali ya kisiasa, madola ya kigeni na vilevile mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya. Mazungumzo hayo yalifanyika mara kadhaa na kwa duru kadhaa pia. Hatimaye mazungumzo hayo yalifikia natija baada ya kufanikiwa kupata utatuzi wa kisiasa wa mgogoro huo.
Kuainishwa tarehe 24 Disemba mwaka huu kama siku ya kufanyika uchaguzi mkuu, kuchaguliwa Mkuu wa Baraza la Uongozi na Waziri Mkuu pamoja na mawaziri wa Serikali ya Muda ya Umoja wa Kitaifa ni miongoni mwa makubaliano yaliyofikiwa na pande husika katika mazungumzo ya Libya. Aidha kwa mujibu wa makubaliano hayo, Abdul-Hamid Dbeibah ndiye Waziri Mkuu wa serikali hiyo ambayo itakuwa na jukumu zito la kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi mwishoni mwa mwaka huu. Serikali hiyo inatakiwa kuandaa mazingira mwafaka ya kufanyika uchaguzi huru, wa haki na kuhakikisha kwamba, wananchi wote wanashiriki uchaguzi huo katika mazingira ya amani na huru kamili.
Katika hatua iliyofuata serikali ya Waziri Mkuu Dbeibah ilifanikiwa kupata kura ya kuwa na imani nayo katika Bunge la nchi hiyo na hivi sasa baada ya kuapishwa hapo jana imeanza rasmi kazi zake.
Aguilla Saleh Issa, Spika wa Bunge la Libya sanjari na kusisitiza kwamba, kuna haja ya kuwekwa kando hitilafu nchini humo amesema kuwa, sasa kimewadia kipindi cha kupeana mikono na kuweko anga ya kusamaeheana baina ya wananchi wa taifa hili moja.
Walibya wana matumaini kwamba, kuanza kazi Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ni mwanzo wa kufikia tamati kipindi cha vita na vitendo vya utumiaji mabavu nchini humo na sasa kumeandaliwa uwanja wa serikali ya wananchi kushika hatamu za uongozi. Kurejesha amani na usalama, kuheshimu makundi mbalimbali makubaliano ya usitishaji vita, kuwafurusha wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh, kuzingatia kwa mapana na marefu suala la uchumi ikiwemo kadhia ya kukarabati miundomsingi ya nchi, uuzaji mafuta ya petroli nje ya nchi, kuvutia wawekezaji na kuboresha maisha ni miongoni mwa mambo mengine ambayo wananchi wa Libya wanataraji kutoka kwa serikali hii mpya.
Himesh Kinner, ambaye ni msomi na mtafiti anasema kuwa, kuingia madarakani Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni habari njema kwa sekta ya mafuta ya Libya ambayo inaweza kunufaika na hilo kwa kuweko uthabiti wa kisiasa. Ugavi wa pato linalotokana na mafuta ya petroli ya Libya ambapo nchi hiyo inafungamana mno na suala hilo, ni kadhia ambayo hadi sasa imekuwa chanzo kikuu cha hitilafu na mivutano baina ya eneo la mashariki na magharibi mwa Libya.
Katika upande mwingine, kufikia tamati uingiliaji wa kigeni na utakaji hisa, hayo nayo yanaweza kuwafungulia njia viongozi wa Libya ili waweze kufanya hima na idili katika mkondo wa maslahi ya taifa na uthabiti wa kisiasa na kijamii wa nchi hiyo. Kama alivyosema Waziri Mkuu Abdul-Hamid Dbeibah ni kwamba, vikosi vya kigeni na mamluki walionunuliwa ni pigo la jambia katika mgongo wa Libya, na ni lazima tufanye juhudi za kuikomboa nchi kutoka mikononi mwao.
Walibya wana matumaini kwamba, kuendelea kuchomoza mwanga wa kisiasa katika nchi hiyo kunaandaa uwanja wa kupatikana mustakabali ulio na tulivu na uthabiti. Hata hivyo wasiwasi wa wingu la hitilafu kutokana na kuweko wingi wa makundi ya kisiasa katika nchi hiyo na uingiliaji wa kimya kimya na usiohisika wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya Libya ukawa kizingiti na kigingi kwa Serikali ya Muda na hivyo kuifanya ishindwe kutekeleza vyema majukumu yake.