Wananchi wa Tunisia waendelea na maandamano ya kulalamikia mgogoro wa kisiasa
(last modified Sun, 21 Mar 2021 12:25:28 GMT )
Mar 21, 2021 12:25 UTC
  • Wananchi wa Tunisia waendelea na maandamano ya kulalamikia mgogoro wa kisiasa

Wananchi wa Tunisia wameendelea na maandamano ya kupinga mgogoro wa kisiasa na matatizo ya kiuchumi na kimaisha nchini mwao.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, waandamanaji wamebeba mabango yaliyoandikwa: "Kuvunjwa Bunge ni jukumu la kitaifa" ikiwa ni kutangaza moja ya malengo ya maandamano yao ya kutaka kufanyika kura ya maoni kuhusu kuvunjwa bunge la Tunisia.

Mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu, Bunge la Tunisia lilipasisha kwa kura nyingi muswada wa marekebisho ya Baraza la Mawaziri la Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Hichem Mechichi. Hata hivyo Rais Kais Saied wa nchi hiyo amekataa kuliapisha baraza hilo la mawaziri akisema sheria za nchi zimekiukwa.

Rais Kais Saied wa Tunisia na Waziri Mkuu, Hichem Mechichi

 

Baada ya mapinduzi ya wananchi ya mwaka 2011 hadi hivi sasa, Tunisia imekuwa uwanja wa maandamano, malumbano na mivutano ya kila namna. Mzozo mkubwa uliopo hivi sasa ni baina ya Rais na Waziri Mkuu.

Nchi hiyo hivi sasa inahitajia mno mazungumzo ya kitaifa. Wananchi wa nchi hiyo wamekuwa wakiandamana mara kwa mara kutaka kuimarishwe misingi ya umoja na mshikamano wa kitaifa, kukomeshwa mizozo baina ya wanasiasa na kushughulikiwa masuala ya kimsingi ya nchi yao hususan masuala ya kiuchumi, ugumu wa maisha, kiwango kikubwa cha vijana wasio na ajira na utulivu na usalama nchini mwao.

Tags