Kamanda wa Libya anayesakwa na ICC auawa kwa kupigwa risasi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i68272-kamanda_wa_libya_anayesakwa_na_icc_auawa_kwa_kupigwa_risasi
Kamanda wa ngazi ya juu huko Libya anayesakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kwa tuhuma za kuhusika na jinai za kivita ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana katika mji wa Benghazi, mashariki mwa Libya.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 25, 2021 03:05 UTC
  • Kamanda wa Libya anayesakwa na ICC auawa kwa kupigwa risasi

Kamanda wa ngazi ya juu huko Libya anayesakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kwa tuhuma za kuhusika na jinai za kivita ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana katika mji wa Benghazi, mashariki mwa Libya.

Mahmoud Mustafa Busayf Al-Werfalli ambaye ni mmoja wa makamanda na wapiganaji watiifu kwa Jenerali muasi Khalifa Haftar aliuawa jana Jumatano baada ya genge la wabeba silaha kulimiminia risasi gari lililokuwa limembeba katika mji wa Benghazi.

Duru za habari zimeliambia shirika la habari la AFP kuwa, kamanda huyo pamoja na binamu yake Ayman, walijeruhiwa vibaya katika ufyatuaji risasi huo, na waliaga dunia wakikimbizwa katika Kituo cha Matibabu cha Benghazi. Hakuna kundi lolote limetangaza kutekeleza au kuhusika na mauaji ya kamanda huyo mtiifu kwa Jenerali Haftar. 

Al-Werfalli ambaye alizaliwa mwaka 1978 ni kamanda wa ngazi ya juu katika brigedi ya al-Saiqa iliyojitenga na Jeshi la Taifa la Libya baada ya kuibuka mapambano ya kumng'oa madarakani dikteta wa nchi hiyo Muammar Gaddafi mwaka 2011. 

Brigedi hiyo imekuwa ikipigana bega kwa bega na wapiganaji watiifu kwa Jenerali Khalifa Haftar huko Benghazi; mji wa pili kwa ukubwa wa Libya ambao ulikombolewa baada ya mapigano ya miaka mitatu.

Werfalli (kulia) na Khalifa Haftar

Majaji wa Mahakama ya ICC mwezi Agosti mwaka 2017 walitoa waranti wa kutiwa mbaroni Al-Werfalli wakidai kuwa alihusika na mauaji ya watu 33 katika mji huo kati ya mwaka 2016 na 2017.

Aidha Julai mwaka 2018, majaji wa ICC walitoa waranti ya kutiwa nguvuni kamanda huyo wa Jeshi la Taifa la Libya (LNA) kwa tuhuma za kuua wafungwa wa kumi mbele ya Msikiti wa Bi’at al-Radhwan mjini Benghazi.