UN yataka mamluki wa kigeni waondoke Libya
-
Ján Kubiš
Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya amewataka wapiganaji wote mamluki wa nchi za kigeni kuondoka katika ardhi ya nchi hiyo.
Ján Kubiš ambaye alikuwa akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kuondoka askari wa kigeni nchini Libya na kutahadharisha kuwa, yumkini kuendelea kuwepo askari hao kukazuia au kupelekea kuakhirishwa uchaguzi wa mwezi Disemba ambao lengo lake ni kuundwa serikali moja katika nchi hiyo iliyoharibiwa na vita.
Kubiš amesema makubaliano ya kusitisha mapigano bado yanaendelea kuheshimiwa lakini wapiganaji mamluki na askari wa kigeni bado wapo katika ardhi ya Libya na kuna ripoti za kuanzishwa vituo vya kijeshi katikati mwa Libya kuanzia mji wa kistratijia wa Sirte hadi al Jufra.
Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya pia ameashiria harakati za kundi la Daesh nchini humo na kutoa wito wa kuendelezwa misaada ya kimataifa kwa maafisa wa Libya kwa ajili ya kupambana na ugaidi na makundi ya waasi, suala ambalo amesema ni la dharura kwa ajili ya kulinda amani na usalama wa nchi hiyo.
Libya ilitumbukia katika mapigano ya ndani mwaka 2011 baada ya kuondolewa madarakani dikteta wa zamani wa nchi hiyo Muammar Gaddafi. Machafuko hayo ya Libya yalichochewa zaidi na uingiliaji wa nchi za Magharibi katika masuala ya ndani ya nchi hiyo