Safari ya mawaziri watatu wa mambo ya nje wa Ulaya nchini Libya
(last modified Sat, 27 Mar 2021 02:30:50 GMT )
Mar 27, 2021 02:30 UTC
  • Safari ya mawaziri watatu wa mambo ya nje wa Ulaya nchini Libya

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Ufaransa, Ujerumani na Italia Alkhamisi iliyopita walikwenda Tripoli mji mkuu wa Libya kwa shabaha ya kujadili mustakbali wa uhusiano wa nchi za Ulaya na Libya. Mawaziri hao pia wamesisitiza udharura wa kuondoka vikosi vya majeshi ya kigeni katika ardhi ya Libya.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Libya, Najla al-Mangoush amesema katika kikao cha waandishi habari kilichowajumuisha pia mawaziri wenzake wa mambo ya nje wa Ufaransa, Ujerumani na Italia kwamba, pande hizo zimeafikiana juu ya ulazima wa kuondoka majeshi ya nchi za kigeni katika ardhi ya Libya na kufunguliwa tena balozi za kigeni nchini humo. Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian amesema lengo ya safari yake na wenzake wa Ujerumani na Italia nchini Libya ni kusisitiza msimamo mmoja wa Umoja wa Ulaya kuhusiana na faili la Libya kutokana na ukaribu wa nchi hiyo na bara Ulaya na athari mbaya za mgogoro wake katika eneo la Sahel, Kaskazini mwa Afrika na Mediterania. Le Drian amesisitiza kuwa, kuna udharura wa kuondoka majeshi ya nchi za kigeni katika ardhi ya Libya kwa lengo la kuimarisha mamlaka ya serikali ya nchi hiyo. 

Safari ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizo tatu muhimu za Ulaya nchini Libya ambazo katika miaka kadhaa ya hivi karibuni zimekuwa na nafasi muhimu katika matukio ya kisiasa ya nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta ya kaskazini mwa Afrika, inaonyesha umuhimu wa Libya na taathira zake za moja kwa moja kwa bara la Ulaya. Suala la kuundwa serikali moja madhubuti nchini Libya na kuimarishwa usalama wa nchi hiyo na hatimaye kuzuia wimbi la wahijiri haramu kutoka Afrika kuingia Ulaya, lina umuhimu mkubwa sana kwa nchi za bara hilo zinazosumbuliwa na tatizo la wahamiaji hususan Italia, Ufaransa na Ujerumani. 

Najla al-Mangoush na mawaziri wenzake wa mambo ya nje wa Ufaransa, Ujerumani na Italia

Katika upande mwingine nchi yenye utajiri mkubwa wa mafuta ya Libya inawavutia mno watu wa Ulaya katika uwanja wa nishati. Mtaalamu wa uhusiano wa kimataifa, Maryam Khaliqi-Nejad anasema: "Libya, kwa nchi za Ulaya, inahesabiwa kuwa miongoni mwa nchi zenye taathira kubwa katika siasa za Afrika na ina nafasi muhimu sana katika baadhi ya masuala ya kimataifa hususan sekta ya nishati." 

Vilevile mgogoro wa Libya umekuwa na taathira mbaya kwa usalama wa nchi za Ulaya. Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ufaransa anasema: "Libya ni jirani yetu na hatuwezi kufumbia macho taathira mbaya za mgogoro unaojiri nchini humo kwa usalama, sekta ya utalii na wimbi la wahajiri barani la Ulaya." 

Nchi ya Libya ilitumbukia katika awamu mpya ya vita vya ndani baada ya linalojiita jeshi la taifa linaloongozwa na jenerali mstaafu, Khalifa Haftari, kuanzisha mashambulizi makubwa Aprili mwaka 2019 kwa shabaha ya kuteka na kuudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli na kuiondoa madarakani Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa. Vita hiyo iliendelea kwa kipindi cha karibu mwaka mmoja na nusu. Kwa kutilia maanani uingiliaji wa nchi za kigeni katika vita hiyo ambazo kila moja inafuatilia maslahi yake binafsi, vita hiyo ya ndani mechukua mkondo mpana zaidi na kutatiza suala la kufikiwa mapatano ya kusitisha vita kutokana na mkinzano wa maslahi baina ya madola yanayoshiriki au kufadhili moja kati ya pande hasimu nchini Libya. Uturuki, Qatar na Italia zimeiunga mkono Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa katika vita hiyo huku nchi za Saudi Arabia, Imarati, Ufaransa na Russia zikimuunga mkono jenerali muasi, Khalifa Haftar. Vita hiyo pia ilifungua mlango wa kutumwa wapiganaji mamluki kutoka nchi za kigeni nchini Libya. 

Vita vya ndani nchini Libya

Sasa Libya imepata serikali moja ambao wadhifa wake mkuu ni kuiongoza nchi hiyo katika kipindi cha mpito hadi wakati wa kuitishwa uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka huu wa 2021. Mapatano hayo yalifikiwa baada ya kutiwa saini makubaliano ya kusitishwa vita. 

Kwa sasa na sambamba na safari ya mawaziri wa mambo ya nje wa nchi tatu za Ulaya zinazohusika kwa njia moja au nyingine na mgogoro wa Libya, inatarajiwa kuwa, Ulaya itachukua msimamo mmoja na kujiepusha na siasa zinazokinzana za hapo awali kuhusiana na Libya hususan baina ya Ufaransa na Italia.